ALIYEKUWA Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Ole Nasha anatarajiwa kuagwa kitaifa kesho katika viunga vya bunge na kusafirishwa siku ya Ijumaa kwa ajili ya maziko yatakayofanyika katika kijiji cha Osinoni kata ya Kakesio wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema Olenasha ataagwa kesho majira ya saa 5:00 katika viunga vya bunge na siku ya ijumaa mwili utasafirishwa kuelekea kijijini kwake.
Amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mawasiliano na Bunge, Familia na Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini katika kikao cha awali familia imeomba azikwe kijijini kwao na kwamba suala hilo halina pingamizi.
“kesho tutafanya buriani ya kitaifa ambayo itashirikisha viongozi wote ambayo itafanyika bunge kwa sasa tunawasiliana na Spika na kiongozi wa dini wa dhehebu alilokuwa anasali na ratiba ikienda vizuri tutaanza saa 5.
Tutampa heshima mpendwa wetu kama kiongozi mwenzetu baada ya hapo safari itaanza siku ya ijumaa na jumamosi mazishi yatafanyika, sisi kama Serikali tutahakikisha viongozi wanaoenda ngorongoro utaratibu unafanyika,”amesema.
Ameongeza: “saa 10 leo tutakutana tena kuona kama kuna jambo la kujadili tena kwenye kikao kuhusu taratibu za mazishi lakini kwa hatua ya mwanzo tumefika hapa,”.
Na SELINA MATHEW, Dodoma