MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Emmanuel Ole Shangai, ameongoza katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kupata kura 420 kati ya kura 940 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege Orkanda Mji Mdogo wa Wasso, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Gerald Munusi, alimtangaza Ole Shangai kuongoza kura za maoni.
Munusi aliwataka wanachama hao, kutoshangilia kwa sababu mchakato wa kuchakata majina unaendelea.
Aliwataja wagombea wengine na kura zao katika mabano ni Joseph Parsambei (187), Elias Ngorisa (136), Sirael Nambololo (61), Dk. Kokel Melubo (56), Moloimet Ole Moko (21), Mesha Singolyo ( 19) na Patrick Kisango (10).
Wengine ni Elizabeth Gibasea (7), Willium Saning’o (7), Daud Haraka (5), Dk. Elifuraha Laltaika (4), Rose Ngilo (3), Elinora Sangei (2), Leyan Sabore (1), Elias Nagol (1) na James Taki (0).
Shangai aliongoza katika kura hizo za maoni, alilishukuru jopo la wasimamizi wa uchaguzi huo na kwamba, huo ni mwanzo wa mchakato, anachosubiria ni uamuzi kutoka katika vikao vya ngazi za juu .
“Ninawashukuru wana CCM wenzangu kwa kura walizonipa na ninalishukuru jopo la wasimamizi wa uchaguzi huu kuanzia ngazi ya makao makuu ya CCM, mkoa na wilaya kwa sababu uchaguzi umekuwa huru na haki,”alisema.
Mmoja wa wanawake walioshiriki uchaguzi huo kati ya wanne, Elizabeth, aliwashukuru wanaCCM kwa kuwaamini wanawake na kuwapigia kura japo hajawangooza katika uchaguzi huo.
“Uchaguzi ulikuwa mzuri na haki. Tumeridhika na matokeo, tunaahidi kumuunga mkono mgombea ambaye jina lake litarudi ili CCM iendelee kuongoza katika jimbo letu la Ngorongoro.”
Naye Mkurugenzi wa uchaguzi huo, Musa Matoroka ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, aliwaonya wagombea kutokufanya kampeni za aina yoyote na wasubiri uamuzi ya vikao vya CCM Taifa.
“Katika uchaguzi, mshindi ni mmoja kwa sababu nafasi ni moja, kushinda kura za maoni si kigezo cha kuteuliwa, hivyo niwaombe muendelee kuwa watulivu wakati vikao vikiendelea,” alisema.
Matoroka alitumia fursa hiyo kuwataka wagombea wote kuvunja makundi, kuungana kuwa kitu kimoja ili jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM litakaporudi, wamuunge mkono katika kampeni.
“Ushindi ni wa CCM si watu. CCM ikishinda ndiyo fahari yetu sote, hivyo niwaombe muungane muwe kitu kimoja kwa maslahi mapana ya Chama chetu”.
Kufanyika kwa kura za maoni unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Ngorongoro ambaye alikuwa Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji ,William Tate Ole Nasha, aliyefariki i ghafla Septemba 27, mwaka huu, nyumbani kwake Jijini Dodoma.
NA LILIAN JOEL, Arusha