MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA), imetangaza kushuka bei ya petroli na mafuta ya taa, huku bei ya dizeli ikiongezeka kwa sh. 13 kwa lita.
Akitoa taarifa hiyo kuhusu mwenendo wa bei za mafuta nchini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje, amesema kushuka kwa bei ya mafuta kumesababishwa na punguzo la bei katika soko la dunia.
“Bei za rejareja za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa shilingi 21 kwa lita (petroli), shilingi 44 kwa mafuta ya taa huku bei ya dizeli ikiongezeka shilingi 13 kwa lita,” amesema.
Chibulunje amesema bei za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimepungua kwa shilingi 123 kwa petroli na shilingi 92 kwa bei ya dizeli.”
Amesema bei za mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kusini zitaendelea kuwa zilezile zilizotangazwa Januari, mwaka huu.
Chibulunje amebainisha kuwa hali hiyo imesababishwa na kutokuwa na shehena ya mafuta yaliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.
“Bei za mafuta ya rejareja za petroli na dizeli katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zitaendelea kuwa zile zile zilizotangazwa mwezi uliopita kwa sababu hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya mafuta ambayo inaweza kubadili bei iliyopo sokoni,” alibainisha.
Katika hatua nyingine, Chibulunje amesema katika kuhakikisha kunakuwa na usawa katika bei mpya zinazoanza kutumika Februari, mwaka huu, ununuaji wa mafuta katika ghala sasa kutakuwa na bei mbili.
Ameongeza kuwa kutakuwa na bei ya kikomo ambayo muuzaji hatakiwi kuzidisha na bei ya chini ambayo muuzaji hatakiwi kushuka zaidi.
Alisisitiza kampuni za mafuta zitakuwa huru kuuza mafuta kwa bei ya ushindani huku wakizingatia bei kuvuka mipaka au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa.
“Katika kuhakikisha kunakuwa na ushindani sawa katika bei zinazoanza kutumika kesho ununuaji wa mafuta katika maghala sasa kutakuwa na bei mbili moja ya kikomo ambayo muuzaji hatakiwi kuzidisha na bei ya chini ambayo vile vile hatakiwi kushuka zaidi,” alisisitiza.
Kuhusu tishio la kupanda kwa bei za mafuta Machi na Aprili, mwaka huu, mkurugenzi huyo alisema katika kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia kuna uwezekano mkubwa bei za mafuta zikaongeza, kutokana na kupanda bei katika soko la dunia.