WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Idara ya Mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi kwa madai ya matumizi mabaya ya fedha.
Akizungumza na watumishi hao, Majaliwa aliwasihii watumishi kufanya kazi za wananchi, siyo kukaa maofisini bila kuwatumikia wananchi hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Watumishi niliowasimamisha kazi ni Bahaye Shilungashela, Mohammed Samadu na Ally Kinyonge wote hawa ni idara ya mapato…
“Niwaombe watumishi mfanye kazi si kula fedha za serikali. Nimewasimamisha hawa kutokana na ulaji fedha za serikali,” alisema Majaliwa.
Amemuagiza Mhazini wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Mudrika Mjungu, kusimamia na kuhakikisha anatengeneza mashine za kielektroniki 55 ambazo zimeharibika, lengo ni kudhibiti wizi wa mapato wa fedha za serikali bila sababu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inafanya kazi ya kukusanya mapato katika maeneo ya halmashauri zote nchini, lakini katika halmashauri ya Kilwa, wamekuwa wezi katika ukusanyaji mapato, hivyo amewasimamisha kazi hao watu watatu.
“Niwaombe watumishi kuweni waadilifu katika fedha za serikali, maana inajitahidi kuleta fedha, kununua mashine za kukusanya mapato katika kila halmashauri, lakini Wilaya ya Kilwa mna mashine 99, ila mashine 55 hazifanyi kazi.
“Sasa mapato mnapeleka wapi, acheni kula fedha za serikali,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amewaasa watumishi wa Kilwa, kukusanya mapato kwa uadilifu wa hali juu na kufuata maadili ya kazi.
Majaliwa amesema: “Kilwa kuna mashine ya kugandishia barafu kwa ajili ya samaki, serikali iliinunua kwa zaidi ya sh. milioni 200, sasa imeharibika, mnataka kuiuza kweli ninyi halmashauri ya ajabu, mnashindwa kutengeneza mashine…Sasa nawaagiza kutengeneza mashine hii ili muendelee kukusanya mapato kikamilifu katika wilaya yenu.”
Pia, Waziri Mkuu Majaliwa, amesema ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, haitaki kusikia fedha ambazo wananchi wanatozwa kisha mtumishi anakula fedha za mapato.
Ametoa rai kwa watumishi wote nchini kuendelea kuwa waadilifu katika kusimamia fedha za serikali na kusimamia miradi kikamilifu, kukusanya mapato mengi katika halmashauri nchi nzima.
Na Sophia Nyalusi, Lindi