WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026, utakaogharimu sh. trilioni 114.8, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia sh. trilioni 40.6 na sekta ya umma sh. trilioni 74.2.
Majaliwa amesema fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wa maendeleo na kwamba kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, anawahakikishia wadau hao kuwa fedha hizo zitapatikana na malengo yaliyowekwa yatatekelezwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 29, mwaka huu, wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Amesema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.
Waziri Mkuu amesema serikali itahakikisha malengo ya Mpango huo yanafikiwa na kwamba serikali haitafumbia macho tabia ya ukwepaji kodi, uzembe kazini, ufujaji wa fedha, rushwa na itaendelea kuenzi ubunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa mpango huo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi, ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.
Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) hapa nchini, Christine Musisi, amesema wananchi, serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi, watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
Na MWANDISHI WETU