POLISI Mkoa wa Mbeya, inawashikilia watu watatu wanaodhaniwa ni majambani kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukutwa na vitu mbalimbali zikiwemo bunduki mbili, risasi 10, bastola na gobole zilizotengenezwa kienyeji.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoani wa Mbeya, Christina Musyani, alisema watuhumiwa hao Msafiri Mwahonje (46), mkazi wa Usangu wilayani Mbarali, Boniface Shupa (36), mkazi wa Matundasi – Chunya na Onesmo Mwachawi (38), mkazi wa Makongolosi ambao walikamatwa Januari 15, mwaka huu, saa 5:45 usiku, mji mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya.
Alisema watuhumiwa hao, walikamatwa katika misako iliyoendeshwa na polisi dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali.
“Watuhumiwa walikutwa na risasi 10 za ‘short gun,’ simu tatu za mkononi, tochi moja, kofia mbili na mizula miwili ambayo hutumia katika matukio ya uharifu,” alisema.
Alisema kwamba, watuhumiwa walihojiwa na kukiri kuhusika katika matukio mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha likiwemo la Januari 2, mwaka huu lililotokea saa 3:30 usiku, eneo la Matundasi.
Christina alisema kuwa, katika tukio hilo, watuhumiwa walivamia duka la mfanyabiashara Andreas John (22), kisha kumpora fedha taslimu sh. milioni 1.1 na vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh.5,490,000 kabla ya kumjeruhi mke wake Sarah Frank (21).
“Januari 14, mwaka huu, saa 2.00 usiku, walivamia duka eneo la Mnazi Mmoja Chunya na kupora fedha kiasi cha sh. 1,925,000, simu za mkononi na vitu mbalimbali,” alisema Christina.
Aliongeza upelelezi wa shauri hilo, unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani.
NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA