WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka vijana wote nchini kuona fahari ya kuzaliwa Tanzania, hivyo waipambanie kuhakikisha inapiga hatua kubwa za maendeleo.
Kabudi, alitoa wito huo hivi karibuni, wakati akizungumza na watumishi wa kada mbalimbali wilayani Iramba, Mkoa wa Singida, alipofanya ziara ya kikazi mkoani hapa.
“Watumishi wenzangu na hasa vijana, oneni fahari mmezaliwa Watanzania na leo hamjazaliwa na makabila yenu, muwe na fahari kwani Tanzania ni taifa, ambalo limejiwekea misingi inayojali watu wote.
“Sisi ni taifa la uchumi wa kati, lililopita katika misukosuko na dhoruba, lakini limebaki kuwa imara na linasonga mbele chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Akieleza lengo la ziara yake wilayani hapo, alisema ni kuona utendaji wa haki, demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria, kama ambavyo imeelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alimuelezea Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, kuwa ni mahiri na ataweza kuingoza kupitia Ilani ya CCM. Awali, akiwasilisha hali ya utendaji wa haki, utawala bora na utawala wa sheria katika wilaya hiyo, Mwenda, alisema Iramba imeendelea kutekeleza shughuli zake kwa kufuata misingi ya utawala bora, kwa kuhakikisha kunakuwepo uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji, utawala wa sheria na majadiliano.
Mwenda alifafanua kuwa wilaya yake imefanikiwa kuhakikisha inawajibika ili wananchi wapate huduma za msingi kwa wakati na kiwango kinachotakiwa.
Alibainisha kuwa serikali ya wilaya imefanikwa kuendesha shughuli zake kwa uwazi na kufanikiwa kuwapa fursa wananchi kupata taarifa muhimu zinazohusu mipango ya maendeleo, huku makusanyo ya fedha na matumizi yake yabandikwa katika mbao za matangazo, hivyo kujua kila kinachoendelea wilayani humo.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Ibrahim Mjanaheri, alimshukuru Waziri Kabudi, kwa namna serikali ilivyorekebisha sheria ya madini na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania.
Pia, alimwomba kutoa kipaumbele cha ujezi wa Mahakama ya wilaya ya kisasa wilayani hapo, kwa sababu itasaidia kutoa taswira nzuri ya wilaya.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, anayeshughulikia Wilaya ya Iramba na Mkalama, Christopher Makwaya, aliseama Mahakama imekuwa na kasi ya kuendesha mashauri kwa njia ya kidijitali.
Makwaya alisema hali hiyo inasaidia kupata nakala ya hukumu muda mfupi baada ya shauri kukamilika na kufanikiwa kusogeza huduma kwa wananchi.
Na MWANDISHI WETU, Iramba