SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknlojia imeitaka Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT kuhakikisha inamaliza ujenzi katika eneo la Iyumbu Jijiji Dodoma kabla ya Februali 2022, kama mkataba unavyoelekeza ili wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi mwakani waweze kujiunga kidato cha kwanza.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Elimu Sayasi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea shule ya Sekondari ya mfano ya Iyumbu iliyopo eneo la Iyumbu na ujenzi wa majengo ya chuo cha Ufundi katika eneo la Nala jijini Dodoma, ili kuona maendeleo ya ujenzi yanavyokwenda katika majengo hayo.
Profesa. Ndalichako ameeleza kuwa shule hiyo inatarajia kutumia kiasi cha Tsh. billion 17 kwa ajili ya ujenzi.
“Nawahakikishia shule hii ikikamilika itakuwa shule nzuri kwa sababu inakila kitu ikiwemo maabara na sehemu za michezo na vitu vingine ambavyo vinahitajika kuwa katika shule,”amesema.
Sambamba na mradi huo, amesema kuna mradi uliokuwa ukifanyiwa kazi kwa muda, ambao ni mradi wa kuimarisha elimu ya sekondari ambapo alisema mradi huo tayari umekwishaanza na fedha zimetolewa kiasi cha US Dolla million 74, ambazo ni sawa na bilioni 170 za kitanzania.
Profesa Ndalichako amesema fedha hizo hizo tayari zimekwishapangiwa matumizi ya kwenda kujenga shule za sekondari kwa ajili ya wasichana ambazo ni za bweni na kwa kuanzia, itaanza mikoa 10 na kila shule itagharamu kiasi cha Tsh. billion nne.
“kutakuwa na shule 184 katika halmashauri ukijumlisha na shule 10 za mfano ambazo zitajengwa katika mikoa 10 itakayojulikana hapo baadae baada ya Waziri wa TAMISEMI atakapotangaza,” amesema
Waziri amesema hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha kuhamisha fedha kwenda katika halmashauri zao, ambapo waziri wa fedha,Tamisemi na Elimu wanahakikisha wanatekeeza agizo la Rais la kuhakikisha ujenzi wa shule unakamilika.
Awali msimaizi wa ujenzi wa mradi wa shule hiyo Luteni Kanali Philemon Komanya amesema, ujenzi wa shule hiyo umefikia asilimia 60, na tayari wameshapokea sh. Bilioni 5.9 za ujenzi huku wakiahidi kutekeleza ombi la Waziri Profesa. Ndalichako kuhakikisha kuwa shule hiyo inakamilika kabla ya Februali 2022 ili wanafunzi wanaohitimu waweze kuanza kusoma hapo mwakani.
Na Happiness Mtweve, Dodoma