MKOA wa Pwani umepokea chanjo nyingine ya Uviko-19 aina ya Sinopharm dozi 25,000 na wananchi wameombwa kuendelea kujitokeza kuchanja.
Akizungumza chanjo hiyo katika kikao cha viongozi wa mkoa kuhusu utekelezaji mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Gunini Kamba, alisema dozi hiyo ni salama na haina madhara hata kwa wajawazito.
“Chanjo hii ya Sinopharm itatakiwa kuchomwa mara mbili, ambapo ukichanja lazima urudie dozi ya pili baada ya siku 28 na hata ukichelewa kurudia baada ya muda huo kwa wiki, haitakuwa na madhara kwani ni lazima uchanje tena
“Katika dozi hii mtu atachanja kichupa kimoja, tofauti na dozi ya Johnson and Johnson ambayo kichupa kimoja kilitakiwa kuchomwa kwa watu watano, “alisisitiza.
Dk. Gunini alisema Halmashauri ya Bagamoyo imepata dozi 4,000, Chalinze 3,000, Kibaha Vijijini 2,000, Kibiti 2,000, Kibaha Mjini 4,000, Kisarawe 3,000, Mafia 1,000, Rufiji 3,000 na Mkuranga dozi 3,000.
Alisema Agosti, mwaka huu walipokea dozi 30,000 ya chanjo, lakini mwitikio haukuwa mzuri kwa kuwa watu walikuwa hawana elimu ya kutosha.
Alisema baada ya wananchi kupewa elimu uchanjaji ulifanikiwa, hivyo mkoa ukaomba nyongeza ya dozi 1,200 ambazo zimemalizika.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema juhudi za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, zimeiwezesha nchi kupata mkopo wenye masharti nafuu sh.trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19.
Alisema hatua za utekelezaji wa mpango huo zimeanza ambapo wataalamu wameshakutana kuandaa mikakati na mipango kazi chini ya usimamizi wa katibu Tawala Mkoa wa Pwani.
Kunenge alihimiza halmashauri kuwa na mpango kazi wenye kuhakikisha utekelezaji unafanikiwa kwa muda uliopangwa.
“Niwatake wananchi waendelee kupambana na ugonjwa wa Uviko-19, tuondokane na vishawishi kuwa chanjo zina madhara, wajitokeze kuchanja na tusimwangushe Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanaasha Tumbo, alielezea Mkoa wa Pwani umeidhinishiwa sh. bilioni 13.3 kwa utekelezaji wa miradi ya elimu na afya.
Pia, zitatumika kujenga vyumba vya madarasa 422 vya shule ya sekondari, vyumba vya madarasa 108 vya vituo shikizi 37 vya shule za msingi, ujenzi wa mabweni manne na nyumba saba za watumishi wa afya, ununuzi wa mashine mbili za mionzi, ICU na ujenzi wa majengo matatu ya huduma za dharura.
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani