CHAMA cha Wafanyakazi Watafiti, Wanataaluma na washirika katika nyanja hizo (RAAWU), kimeipongeza serikali kwa kuyafungulia magazeti manne yaliyofungwa kwa kukiuka maadili, na kusema, hatua hiyo imerejesha fursa kwa wafanyakazi ambao waliathirika kwa kukosa ajira.
Kimepongeza uamuzi huo wa serikali kupitia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, kikisema mbali na kuwarudishia ajira waliokuwa watumishi, pia imedhihirisha kujali na kuona umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, Jane Mihanji, amesema chama hicho kimepokea kwa furaha taarifa ya kufunguliwa kwa vyombo hivyo vya habari.
“Kipekee tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alipoingia madarakani tu, alionyesha kutotaka kusikia uhuru wa vyombo vya habari unaminywa na aliagiza vyombo vilivyofungiwa vifunguliwe,” alisema Jane.
Kwa mujibu wa Jane, magazeti yaliyofunguliwa ni Tanzania Daima, Mwanahalisi, Mawio na Mseto ambayo baadhi yao yalifungiwa miaka minne iliyopita.
Alisema wanatambua kwamba sekta ya habari imekuwa chanzo cha ajira kwa vijana nchini na uwepo wa magazeti hayo, itaendelea kutoa fursa hizo kwa Watanzania.
Jane alieleza uwepo wa umuhimu kwa serikali kuboresha mahusiano kati yake na sekta ya habari kwa kuziboresha sheria na kanuni ambazo zimekuwa kikwazo kwa wanataaluma, ili kurahisisha katika utendaji kazi.
Aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari na wanataaluma hiyo, kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, weledi na maadili ya uandishi kwa ustawi wa tasnia ya habari nchini.
Aidha, mwenyekiti huyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari kuruhusu na kuhakikisha uwepo wa matawi ya vyama vya wafanyakazi katika taasisi zao, ili kurahisisha utetezi wa maslahi yao pindi watakapopatwa na changamoto.
“Hivi karibuni kuna chombo cha habari wafanyakazi wake waliitisha mkutano na wanahabari na kudai kulipwa stahili zao, kweli walifanikiwa na mwajiri aliwalipa, lakini wangekuwa na tawi la chama cha wafanyakazi tatizo lingetatuliwa mapema wasingefikia kule,” alisema.
Jane alisisitiza kwamba wafanyakazi wa taasisi yoyote ya habari wana haki kisheria kuanzisha tawi la chama cha wafanyakazi, sehemu ya kazi, kwani ni takwa la kisheria na mfanyakazi yuko huru kujiunga na chama anachokitaka.
Kauli hiyo ya RAAWU inakuja ikiwa ni wiki moja tangu Waziri Nape avirudishie leseni vyombo vya habari vya Tanzania Daima, Mwanahalisi, Mawio na Mseto, vilivyofungiwa kwa sababu mbalimbali.
Waziri Nape alifanya hivyo, katika mkutano wake na wahariri wa Vvombo vya habari, akisema utekelezaji wa hilo unatokana na maelekezo ya Rais Samia.
Pamoja na RAAWU, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), lilipongeza uamuzi huo wa serikali likisema ni ishara nzuri kwa uhuru wa habari nchini.
Na JUMA ISSIHAKA