MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, imewatia hatiani raia sita wa Rwanda kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria na kuamuru kutaifishwa basi la abiria la kampuni ya Suden’s kuwa mali ya serikali.
Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama hiyo na Hakimu Christina Chovenye, ambapo washitakiwa hao walipewa adhabu ya kulipa faini ya sh. milioni tatu ama kutumikia kifungo cha miezi mitatu gerezani.
Pia Hakimu Chovenye aliagiza kutaifishwa basi la abiria la Kampuni ya Suden’s lenye namba za usajili T.478 DEH aina ya TATA, lililokuwa likiwasafirisha washitakiwa hao kutoka Wilayani Kahama kwenda Mkoani Tabora na kuwa mali ya serikali.
“Washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na wamekiri kosa lao, hawajaisumbua Mahakama. Lakini kwa kuwa makosa haya yamekithiri katika jamii hii watalipa faini ya shilingi 500,000 kila mmoja, wakishindwa watafungwa jela miezi mitatu ili iwe fundisho kwao na jamii kwa ujumla
“Lakini pia Mahakama hii inaagiza kutaifishwa gari aina ya TATA lenye namba za usajili T.478 DEH lililokuwa likiwasafirisha washitakiwa na kuwa mali ya serikali na litatunzwa katika ofisi ya Uhamiaji ya wilaya,” alieleza Chovenye.
Washitakiwa walioanza kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi mitatu baada ya kushindwa kulipa faini ni Japhet Ntakirutimana, Charles Bugingo, Bunan Jeanfelix, Mugisha Pasifique, Kubwimana Gaspard na Nshiyimana Denis.
Awali, Mwendesha Mashitaka, Satuninus Kamala alidai washitakiwa hao Novemba 11, mwaka huu, walikamatwa mchana na maofisa uhamiaji eneo la Kagongwa wilayani Kahama wakiwa nchini pasipo vibali halali.
Alidai washitakiwa hao walikamatwa wakiwa ndani ya basi la Kampuni ya Suden’s lililokuwa linakwenda mkoani Tabora wakitokea Kahama, ambapo ilibainika ni raia wa kigeni kwa kuwa hawakuwa na vibali halali vinavyowaruhusu kuingia nchini.
Alidai baada ya washitakiwa hao kukamatwa walifikishwa katika kituo cha Polisi cha Kahama na walikiri kuingia nchini pasipokuwa na vibali halali.
Na Chibura Makorongo, Shinyanga