RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania wasiridhike na yaliyofanywa na serikali yake katika siku 100 za uongozi wake na kwamba kazi iendelee kwa kasi ili kujenga taifa.
Amesema anahitaji muda zaidi ili kuketi na viongozi wa vyama vya upinzani na kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo katiba, kwa kuwa yapo mambo mengine muhimu zaidi ya hayo.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Ikulu ya Dar es Salaam, wakati akizungumza na wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, katika siku 100 za uongozi wake madarakani.
“Ndugu zangu sasa hivi nchi yetu ina changamoto nyingi sana, tuna janga la covid linatupiga, kuna uchumi umeshuka inatakiwa kuupandisha, tuna mambo mengi ya kushughulikia hapa.
“…Nimeanza kukutana na wenzangu mmoja mmoja, baadaye tutakutana na makundi hebu niombe sana Watanzania, kama inavyosemwa nimeanza vizuri, naomba nipeni muda nisimamishe nchi kiuchumi,” alisema.
Rais amesema muda ukifika katiba itazungumziwa pamoja na mikutano ya hadhara, huku akisisitiza kuwa hata sasa, serikali imeruhusu shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya ndani ya vyama vya siasa na mikutano ya hadhara ya wabunge katika maeneo yao.
Kadhalika, amesema kesho anatarajia kupokea taarifa ya uchunguzi aliyoagiza ufanyike kuhusu miamala ya fedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika miezi miezi mitatu ya mwanzo, kuanzia Januari, mwaka huu.
Taarifa hiyo ni ile aliyomuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), afanye uchunguzi katika ofisi hiyo nyeti kwenye uchumi wa nchi, ili kujiridhisha na yaliyokuwa yakivumishwa mitandaoni.
Rais amesema kazi ya Urais ni ngumu, lakini anaiweza barabara kwa sababu nafasi hiyo ni taasisi yenye vyombo vingi vya kutekeleza majukumu, lakini inahitaji maamuzi ya kila jambo baada ya kuchakatwa.
Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari nchini, ikiwemo kuketi na wahariri mara mbili kwa mwaka, ili kuhakikisha vinakuwa na mchango chanya kwenye maendeleo ya taifa.
Rais katika mazungumzo hayo na wahariri, amevishukuru vyombo vya habari na wanahabari wote kwa ushirikiano alioupata tangu alipokula kiapo cha kushika wadhifa huo, Machi 19, mwaka huu.
Akijibu maswali ya wahariri, Rais aligusia masuala kadhaa kwa ujumla, yakiwemo maambukizi ya virusi vya corona, kufunguliwa kwa magazeti yaliyofungiwa, uteuzi wa vijana zaidi ya wazee na hali ya uchumi wa vyombo vya habari na taifa kwa ujumla.
Kuhusu corona, Rais amesema kazi aliyoitoa kwa tume maalumu aliyoiunda, ili kushughulikia uhalisia wa maambukizi ya virusi hivyo nchini, imekwenda vizuri na kuijadili katika baraza la mawaziri, siku chache zilizopita na kwamba hadi sasa, Tanzania ina wagonjwa kama 100 na kitu wa corona.
“Tumeamua tufanye kama wanavyofanya wenzetu duniani, tuchanje, lakini tuchanje kwa hiari, tunafanya hivi kwa sababu Watanzania wengi wafanyabiashara wamechanja nje ya nchi, tukasema chanjo sasa itakuwa si lazima ni hiari ya mtu,” alisema.
Aidha, amesema mapambano ya corona si ya serikali pekee, bali pia wananchi ambao wanatakiwa kuhakikisha wanachukua tahadhari mahali walipo kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya.
Rais Samia amesema hadi sasa, mashirika mengi ya kimataifa yamejitokeza kuisaidia Tanzania kwenye masuala yanayohusu chanjo na kwamba kuna takriban sh. trilioni 1.1, kwa ajili ya mapambano hayo.
“Wananchi kwa ujumla wetu, tujikinge na tuchukue tahadhari zote…Kingeni sana watoto, kila mmoja na familia yake,” alisisitiza.
Kufunguliwa kwa magazeti
Rais amesema kwa taarifa aliyonayo, baadhi ya magazeti yamemaliza kutumikia adhabu yao na kwamba ili yarudi kwenye biashara, yanahitaji kusajili upya leseni zao.
Amesema hata hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari kufuata sheria na utaratibu kwenye kufanya kazi ili kuendelea kutimiza majukumu yake katika jamii.
“Tukosoeni kama serikali na tuonyesheni na njia na sisi tutajitokeza na kuomba radhi,” alisema.
Ameahidi kuendelea kulipa kwa awamu madeni ambayo serikali inadaiwa na vyombo vya habari, huku akisisitiza kuwa lazima madeni hayo yahakikiwe.
Mmoja wa wahariri waliopata nafasi ya kuuliza maswali kwenye mkutano huo, ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group (UMGL), Ernest Sungura, ambaye alitaka kujua mambo yanayomtia moyo kwenye Urais katika siku zake 100 za uongozi wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, amesema wizara yake inajivunia utendaji wa Rais katika siku 100 madarakani ikiwemo kuipendelea sekta ya habari, michezo na sanaa kupitia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amesema wako katika hatua za mwisho za kuanzisha bodi huru ya ithibati ya wanahabari, ambalo litashughulikia changamoto za wanahabari kote nchini.
Waziri huyo amesema katika kulifanikisha hilo, wamefikisha ombi maalumu kwa Katibu Mkuu Kiongozi, ili kutoa fursa ya kuteuliwa kwa wajumbe wa bodi hiyo.
Na WILLIAM SHECHAMBO