RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza vijana kujiunga na mabaraza ya vijana, ili kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana.
Amesema huu ni wakati vijana kufanya hivyo, kwa kuwa watanufaika na fursa hizo zilizolenga kuwaletea mabadiliko makubwa ya kimaisha.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipozungumza wakati wa matembezi ya kuyaenzi mapinduzi matukufu ya Zanzibar, yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
Alisema serikali ya awamu ya nane imejipanga kuliwezesha kundi la vijana kiuchumi, kwa kuwa ni maalumu na lenye changamoto nyingi.
Alibainisha kuwa kwa kutambua changamoto zinazowakabili vijana, serikali imejipanga kuwawezesha kupitia mifuko ya uwezeshaji kiuchumi na kuona inaleta tija.
Kutokana na hilo, aliwataka vijana kuyatumia na kujiunga na mabaraza ya vijana ambayo miongoni mwa majukumu yake makubwa ni kuwaunganisha na kunufaika na fursa za uwezeshaji kiuchumi.
”Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imejipanga kuwaunganisha vijana wote kwa kujiunga na mabaraza ya vijana ili kunufaika na fursa za kiuchumi za uwezeshaji, hatua ambayo itawawezesha kubuni miradi ya maendeleo,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka vijana wa CCM kuyaenzi mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964 ambayo ndiyo yaliyowakomboa wananchi wa Zanziba na wazalendo kushika dola.
Alisema miongoni mwa kundi ambalo linawajibika kuyalinda mapinduzi hayo ni la vijana kutokana na nguvu zao, huku wakifaidi matunda yake katika sekta za elimu na huduma za afya bure.
“Haikuwa kazi nyepesi ya wazee kufanikiwa kufanya mapinduzi, ambapo busara, umoja na dhamira ya dhati ndiyo nguzo na dira ya kufanikisha mapinduzi hayo,” alisema.
Aliongeza kuwa: “’Vijana nyinyi ndiyo nguzo ya kuyalinda mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, ambapo matunda yake yanayotokana na kupatikana kwa huduma za kijamii bure, sasa ndiyo mnanufaika nayo kikamilifu.’
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Mussa Haji, alisema wapo vijana imara huku wakiridhishwa na utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuona maendeleo yanafikiwa kwa wananchi.
”Vijana wa CCM tumeridhishwa na uongozi wa viongozi wetu wakuu wa kitaifa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa jinsi wanavyoongoza, kwa kuwa wamelenga kuwakomboa wananchi kiuchumi na kimaendeleo,’ alisisitiza.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Sadalla, alibainisha kuwa Chama kimeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na UVCCM katika kuhakikisha Chama kinakuwa imara na kuingiza wanachama wengi.
Aliwataka vijana kamwe wasikubali kudanganywa kuhusu mapinduzi hayo kwa kuwa yaliwakomboa wananchi wa Zanzibar kwa kuuondoa utawala wa kigeni wa Sultani.
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR