RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati nchi ikijiandaa kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kuna fursa nyingi za uwekezaji.
Rais Mwinyi aliyataja maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kuwekeza kuwa ni pamoja na uchumi wa buluu, mafuta, gesi na utalii.
Pia Rais Mwinyi aliwahamasisha wawekezaji kwenda kuwekeza Zanzibar kupitia maeneo hayo kwa kuwa bado hayajatumiwa ipasavyo.
Rais Mwinyi aliyasema hayo jana, wakati akifungua kongamano la uwekezaji ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru liliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Unguja.
Alisema sekta hizo zina fursa nyingi Zanzibar kwa kuwa lengo la serikali ni kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji kwa maslahi ya nchi.
Alieleza serikali imeanzisha taasisi za kusimamia uwekezaji kwa kuweka sera, sheria na miongozo mizuri katika sekta hiyo ili wawekezaji wasipate vikwazo wanapotaka kuwekeza nchini.
Rais Mwinyi alitaja maboresho hayo ni kutungwa sheria ya kuhamasisha na kulinda uwekezaji ya mwaka 1990, ambayo iliwezesha kuanzishwa taasisi ya kuhamasisha uwekezaji na sheria iliyotungwa mwaka 1996 na sheria ya uwekezaji ya mwaka 1997.
Rais Mwinyi, alisema serikali ilianzisha sheria mbalimbali za kukuza uchumi na kuondokana na changamoto ya utegemezi wa mazao ya biashara yakiwemo karafuu, nazi, pilipili na viwanda walivyorithi kutoka serikali ya mkoloni.
Dk.Mwinyi alisema serikali iliboresha mazingira ya uwekezaji kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ambapo mwekezaji akikamilisha taratibu ndani ya siku tatu anapata kibali ikiwa na mpango wa kutoa kibali ndani ya saa 24.
Aidha, alisema katika kutatua tatizo la upatikanaji wa ardhi, serikali inakamilisha utaratibu wa kuwa na benki ya ardhi baada ya kubainisha maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji.
Pia Rais Mwinyi alisema serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya mafuta na gesi na amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo ili kukuza uchumi wa Zanzibar na kutoa fursa za ajira.
Katika kutoa fursa za uwekezaji, serikali imetenga visiwa vidogo 10 vilivyopo Zanzibar kwa ajili ya kuwekezwa katika sekta ya utalii ambayo ndiyo msingi wa kukuza uchumi wa nchi.
Rais Mwinyi alisema serikali itachukua hatua wananchi washiriki kikamikifu katika kuwekeza na badala kuwa watazamaji na amezitaka jumuiya za wafanyabiashara kuwa karibu na serikali kutumia fursa zilizopo.
Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, alipongeza hatua mbalimbali za kukuza uchumi wa nchi zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Mwinyi.
Karume alisema kitendo cha kuandaa kongamano hilo kinathibitisha dhamira ya viongozi hao ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan kupitia sekta ya uwekeaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, alisema ni muhimu kutumia fursa ya uwekezaji kwa kuwa ndio msingi wa ukuzaji wa uchumi wa nchi na pato la mtu mmoja mmoja.
Alisema wawekezaji wanahitaji kutegenezewa fursa nzuri kwa kuboresha maeneo ya makusanyo ya kodi hatua itakayoinua uchumi kwa nchi kwa sababu Tanzania ina rasilimali za kutosha.
Waziri huyo alisisitiza serikali itaendelea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara, elimu, afya, maji na umeme.
Na EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR