RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza haja kwa nchi za Bara la Afrika kuhakikisha zinafanya biashara pamoja badala ya kuelekeza nguvu zaidi nje ya bara hilo, hatua ambayo itaimarisha uchumi na kuleta maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za Afrika, unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Inkosi Albert Luthuli, KwaZulu-Natal, Jijini Durban, nchini Afrika Kusini.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ili kuweza kufikia azma iliyokusudiwa ni muhimu kutekeleza malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), ambapo katika utekelezaji wake alihimiza haja ya nchi wanachama wa (AfCFTA) kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto zilizopo ambazo ni kikwazo kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji.
Alizitaja miongoni mwa changamoto zinazozifanya nchi za Afrika zishindwe kufanya biashara baina yao, kuwa bado zina vikwazo vingi vinavyosababisha kiwango cha biashara kuwa kidogo baina yao, ikiwa ni pamoja na ufinyu wa miundombinu kati ya nchi zenyewe, utatanishi uliopo kuhusu viwango vya ushuru, migongano ya sheria na uhaba wa bidhaa zinazozalishwa.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba lengo la Mkutano pamoja na Maonyesho hayo ya Biashara ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi za Afrika, hivyo kuna kila sababu ya kutiliwa mkazo na kufanyiwa kazi ipasavyo azma hiyo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba kiwango cha kufanya biashara baina ya nchi za Afrika, bado ni kidogo na badala yake sehemu kubwa ya biashara inafanywa katika nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya na Marekani.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa washirika wa mkutano huo kutilia mkazo na hatimaye kuonyesha njia bora za kukabiliana na hali hiyo.
Alisema ni wajibu wa nchi za Afrika kuhakikisha kwamba zinachukua hatua madhubuti ili kuondoa changamoto zilizopo.
Akitoa hotuba yake hiyo, katika uzinduzi wa Mkutano huo, Rais Dk. Mwinyi, alizieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Rais Dk. Mwinyi alieleza hali iliyopo hivi sasa ambayo bado nchi za Afrika zinaendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hata zile ambazo zingeweza kuzalishwa na wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika nchi hizo.
Alisema kwamba Tanzania hivi sasa imeanzisha miradi mikubwa ya maendeleo inayohusu ujenzi wa miundombinu ya bandari na reli kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo ili kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alibainisha utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na vikwazo vyote ambavyo vinarejesha nyuma maendeleo ya biashara katika nchi za Afrika.
Alisema Tanzania imeshasaini Mkataba wa kuwa mwanachama wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), kwa hivyo, itahakikisha inatekeleza malengo na mikakati iliyowekwa ili kuyafikia madhumuni yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kwa eneo hilo.
Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza viongozi na wananchi wa Afrika ya Kusini kwa makaribisho yao na ukarimu mkubwa waliouonyesha kwa ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kwake yeye binafsi.
Sambamba na hayo, katika suala zima la Maonyesho ya Biashara, Rais Dk. Mwinyi, alisema maonyesho hayo yana umuhimu mkubwa katika kukuza maendeleo ya biashara barani Afrika.
Kwa upande wao, marais na viongozi kutoka nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo, walipata fursa ya kueleza mikakati na juhudi zinazochukuliwa na nchi zao katika kuhakikisha suala zima la biashara huria linapewa kipaumbele katika bara la Afrika ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana, huku wakieleza athari za UVIKO 19 zilivyorejesha nyuma hatua hiyo.
Naye, Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo, aliwakaribisha wageni wake wote aliowaalika huku akieleza mikakati ya nchi yake na kueleza utayari kwa nchi hiyo katika kutoa ushirikiano juu ya suala hilo.
Na Mwandishi Maalum