RAIS wa Zanzibar na Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano utakaojadili masuala ya kuzuia na kudhibiti vitendo vya ufisadi nchini.
Mkutano huo utafanyika Desemba 13-15 Zanzibar na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 ambao ni wahasibu, wakaguzi wa ndani, wakuu wa taasisi, wachunguzi na wanasheria.
Pia, mkutano huo umeandaliwa na taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Ufisadi, Rushwa na Ubadhilifu (ACFE), kwa lengo kusaidia taasisi za serikali na zisizokuwa za serikali, kubaini na kuzuia viashiria vinavyosababisha kutokea kwa ufisadi, rushwa na ubadhilifu ili kupunguza hasara inayotokana na vitendo hivyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa ACFE Nchini, Musomi Maira amesema kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo kwa mataifa, imeonesha taasisi zimekuwa zikipoteza asilimia tano ya mapato kutokana na vitendo vya ufisadi, rushwa na ubadhilifu.
“Katika ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar imeonesha kuwepo na vitendo vya ufisadi na ubadhilifu ambavyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara, hivyo kwa kuzingatia hali ilivyo taasisi hii imedhamiria kushirikisha na serikali kuzalisha wataalamu kwenye taasisi mbalimbali ili kubaini na kuzuia kabla havijatokea,”alieleza.
Alisema wameamua kuisaidia serikali kubaini viashiria hivyo mapema ili kupunguza mzigo kwa taasisi nyingine.
“Mara nyingi viongozi wetu wa serikali wamekuwa wakikemea vitendo hivyo kila mara kwa sababu vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo.
“Kwa mfano kwa upande wa Zanzibar wana ajenda ya uchumi wa buluu na ajenda hiyo itafanikiwa endapo tutapinga vita vitendo vya ubadhilifu na ufisadi nchini,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya ACFE Nchini na Rais wa Taasisi ya Nina Tanzania, Bosco Bugali alisema serikali imekuwa ikijitahidi kupambana na vitendo hivyo.
Pia alisema watakuwa bega kwa bega na serikali kudhibiti vitendo, hivyo kwa kutoa elimu ili iwafikie Watanzania wengi.
Na ATHNATH MKIRAMWENI