TANZANIA na Misri zimekubaliana kushirikiana katika maeneo makuu matano ya kimkakati, uamuzi ambao umefikiwa katika kikao cha Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi.
Katika mkutano huo uliofanyika jana jijini Cairo, Misri, ambako Rais Samia yuko katika ziara ya kiserikali ya siku tatu, Rais alianika na kuzinadi fursa za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, huku akimweleza Rais Al-Sisi, kwamba Tanzania kuna mazingira salama ya kiuwekezaji.
MAENEO MAKUU YA USHIRIKIANO
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, iliyotolewa jana, iliyataja maeneo hayo makuu ya kimkakati waliyokubali kushirikiana kuwa; ni katika nyanja za elimu, nishati, michezo, ulinzi, ushirikiano na kuendeleza Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), iliyoanzishwa mwaka 1989.
Katika mkutano huo, Rais Samia alimpongeza Rais Al-Sis kwa kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika taasisi za elimu ya juu nchini humo, kama lugha ya kimkakati na kumuahidi kutuma timu ya wataalam kutoka Tanzania kuisaidia Misri kufanikisha lengo hilo.
“Nakushukuru Rais Al-Sis kwa ushirikiano uliopo wa kijeshi, ambapo watalaam wengi kutoka Tanzania wameendelea kupata mafunzo mbalimbali ya kijeshi nchini hapa,’’ alisema Rais Samia.
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Awali, katika mkutano wao na waandishi wa habari, Rais Samia akiwa na mwenyeji wake, Rais Al-Sis, alisema: “Tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika ajenda kubwa ya usalama wa nchi zetu kwa kuimarisha usalama, amani na utulivu kwa kushirikisha majeshi yetu kupambana na ugaidi,”alisema.
Rais Samia, alieleza kuwa wameona haja ya ushirikiano wa nchi hizo katika suala mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika.
Alimuahidi Rais Al-Sis kuwa, atahakikisha makubaliano yaliyofikiwa baina yao kwa maslahi ya nchi zao yanasimamiwa ipasavyo na serikali yake, yakiwemo ya mikataba iliyosainiwa na wasaidizi wao mapema kabla ya mkutano huo.
FURSA ZA KIBIASHARA NA KIUWEKEZAJI
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari,pia, Rais Samia alizitaja fursa za kibiashara na kiuwekezaji zilizopo Tanzania katika sekta ya madini, nishati, kilimo, utalii, mifugo, usafirishaji na usindikaji wa mazao.
Rais Samia alisema milango iko wazi kwa nchi hiyo kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania ina mazingira bora na usalama wa kutosha , hivyo aliwaomba wawekezaji wa Misri kuja nchini kuwekeza katika maeneo hayo.
Rais Samia alisema Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano na Misri na imefungua milango ya uwekezaji katika maeneo muhimu, ili kuimarisha maendeleo ya kidiplomasia, uchumi, jamii na siasa kwa nchi hizo.

“Tanzania zipo fursa nyingi za uwekezaji nikaribishe wafanyabiashara wa Misri kutumia fursa hiyo, tunayo maeneo muhimu kama ya madini, nishati, kilimo, mifugo, usafirishaji na usindikaji mazao, karibuni sana muwekeze ”alisema.
Rais Samia alisema katika mazungumzo yake na Rais Al Sis, wamekubaliana kushirikiana katika miradi ya maendeleo ili kuimarisha diplomasia ya nchi hizo, uchumi, siasa na jamii.
Alisema katika hatua hiyo wamehakikisha miradi ya kimkakati iliyopo inaendelezwa hususan inayogusa sekta ya utalii, elimu, uchumi, nishati na huduma za kijamii.
“Ushirikiano wa Tanzania na Misri ni wa kihistoria tangu enzi za waasisi wetu; Hayati Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser, na umeendelezwa katika awamu zote za uongozi, mimi na kaka yangu (Al-Sis) tunaahidi nchi hizi mbili zitaendeleza yote mazuri kwa maslahi ya wananchi wake,”alisema.
Rais Samia alisitiza kuwa ushirikiano huo umekuwa na matokeo chanya; ambapo Tanzania inajivunia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Misri katika mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ambapo Megawati 2,155 zitazalishwa.
Alisema kwa pamoja wamezungumzia namna ya kumaliza changamoto zilizopo katika ujenzi wa mradi huo wa kimkakati, ambao unatekelezwa na kampuni kutoka Misri, ili uweze kukamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mbali na uwekezaji huo Tanzania pia zipo fursa nyingi katika sekta ya nishati, ambapo Misri wanaweza kuzitumia.

Rais Samia alieleza namna nchi hizo mbili ambavyo zimekuwa zikinufaika na uwekezaji katika sekta ya afya na elimu, ambapo miradi mbalimbali imekuwa ikitekelezwa.
“Wataalamu wetu wameendelea kubadilishana uzoefu lakini, pia tumekuwa tukiendeleza ushirikiano katika sekta ya elimu, ambapo tumekuwa tukinufaika na ufadhili wa masomo kwa Watanzania wanaokuja Misri,”alisema.
Pia. Rais alisema katika mazungumzo yao wameona umuhimu wa kuongeza fursa za kibiashara, ambapo kwa hivi sasa fursa za biashara zimeongezeka kutoka sh. bilioni 84.3, mwaka 2018 hadi sh. bilioni 87.3, mwaka 2020.
Akizungumzia uwekezaji wa Misri nchini, Rais Samia alisema Misri imewekezaTanzania katika mitaji 26 yenye thamani ya Sh. trilioni 3.1, na kutengeneza ajira 2,206.
Alieleza kuwa nchi hizo kwa pamoja zikiendelea kushirikiana katika sekta hizo za kimkakati na kuimarisha mifumo ya kiteknolojia zitafanikiwa kuimarisha uchumi.
Rais Samia alitumia fursa hiyo kumualika Rais Al Sis kuja nchini Tanzania, lengo likiwa ni kuendeleza ushirikiano uliopo kwa maslahi ya wananchi wa nchi hizo.
Mariam Mziwanda na William Shechambo