RAIS Samia Suluhu Hassan, ameanika mafanikio ya maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyopatikana katika kipindi cha miezi sita tangu Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza ilipoingia madarakani.
Katika kipindi hicho cha kuanzia Machi hadi Septemba, mwaka huu, serikali imefanikiwa kutekeleza miradi makubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu na utoaji huduma za jamii kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma katika uzinduzi wa Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko – 19, Rais Samia alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia kwa kumshukuru Mungu kutokana na taifa kuendelea kupiga hatua muhimu kimaendeleo.
“Miezi sita haikuwa kazi nyepesi, awamu ya sita iliingia madarakani kwa mazingira ya kipekee kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais Hayati Dk. John Magufuli kwa sababu hiyo, mimi na wengine waliopo serikalini, hatukuwa tumejiandaa na tukio hilo,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa: “Kwa hakika, Watanzania tuna sababu ya kumshukuru Mungu na kujipongeza kwa kuvuka mtihani huo salama, siyo mataifa mengi yangeweza kuvuka. Wapo wengine wangeweza kuingia katika machafuko, nawapongeza Watanzania kwa utulivu.”
Katika hotuba yake, Rais Samia alitumia saa moja na dakika nne kueleza mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miezi sita ya uongozi wake.
AMANI NA USALAMA
Rais Samia alisema uwepo wa amani na usalama ndiyo msingi mkuu wa maendeleo kwa taifa uliochangia uwepo wa maendeleo hayo.
Alisema wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa dini, wamekuwa wakishirikiana katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kutawala nchini.

MUUNGANO
Katika kulinda na kudumisha muungano, Rais Samia, alisema katika kipindi cha miezi sita, serikali imefanikiwa kutatua changamoto 11 za kero za Muungano.
Alizitaja baadhi ya changamoto zilizotatuliwa ni usimamizi na ukokotoaji wa kodi katika huduma za simu unaofanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Sheria ya Uvuvi katika ukanda wa uvuvi wa bahari kuu.
Zingine alizozitaja ni ucheleweshaji wa mikataba ya miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa barabara ya Chakechake-Wete na ujenzi wa Hospitali ya Binguni ambapo sasa mikataba hiyo inaendelea kufanyiwa kazi.
“Hakuna shaka kutatuliwa kwa kero hizo kumeimarisha Muungano wetu,” alisisitiza Rais Samia.
UCHUMI
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya uchumi, alisema katika hotuba yake bungeni aliyoitoa Aprili mwaka huu, alizitaja hatua za kuchukua kuimarisha uchumi kwa kuhakikisha viashiria vya uchumi wa jumla vinabaki kuwa imara.
“Nafarijika katika miezi sita iliyopita tumetekeleza yote, mathalani kuhusu usimamizi wa viashiria va ukuaji uchumi wa jumla, ukuaji wa pato la taifa katika robo ya pili mwaka huu kuanzia Aprili mpaka Juni, uchumi umeongezeka kufikia asilimia 4.3, ukilinganisha na asilimia nne kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita,”alisema.
“Tumeweza kudhibiti mfumuko wa bei ambao umeendelea kuwa tarakimu moja. Katika kipindi cha Aprili hadi Septemba mwaka huu mfumuko wa bei umekuwa kwa wastani wa asilima nne,” alieleza.
Kwa upande wa akiba ya fedha za kigeni, Rais Samia alisema hadi Agosti mwaka huu, akiba ya fedha za kigeni imefikia dola bilioni 5.8 zinazoweza kutosheleza kuagiza bidhaa kutoka nje kwa kipindi cha miezi sita, ikilinganishwa na akiba ya dola bilioni 4.9 mwaka uliopita kipindi kama hicho.
Aidha, alisema ukusanyaji mapato ya serikali unakwenda vyema ambapo kuanzia Aprili hadi Septemba mwaka huu, serikali imekusanya sh. trilioni 9.9 huku mapato yasiyokuwa ya kodi yaliyokusanywa yalikuwa sh. trilioni 1.4 na kufikisha jumla ya sh. trilioni 11.4.
Rais Samia alieleza kuwa katika kipindi hicho, serikali imetoa sh. trilioni 8.2 kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pia, alisema serikali imetatua kero ya muda mrefu ya kurejesha marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya sh. bilioni 451.3, kendelea kulipa madeni ya ndani na nje ya nchi, kuhakiki madeni ya ndani ya sh. bilioni 439 ya watumishi wa umma, wazabuni, wakandarasi na huduma za umeme, maji na simu kwa ofisi za umma.
Rais Samia alisema madeni hayo yote yameanza kulipwa na mengine yanaendelea kulipwa katika kipindi cha miezi sita ijayo.

BIASHARA
Kuhusu uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara, alisema serikali imeondoa urasimu katika utoaji vibali vya kazi kwa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa utoaji vibali ambao umeondoa muda wa utoaji vibali kutoka siku 14 hadi siku moja hadi tatu.
Kadhalika, alieleza serikali imekamilisha michakato wa kuunda dirisha moja la kielektroniki la uwekezaji, kituo cha mawasiliano ya uwekezaji, kanzi data ya ardhi na kuimarisha majadiliano na sekta binafsi kwa kufanya mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara.
“Kutokana na hatua hizo, tumesajili miradi yenye thamani ya dola bilioni 3.5 ambayo inatarajia kuzalisha ajira 43,782, miradi 164 yenye thamani ya dola bilioni 3.1 imesajiliwa TIC na EPZA, ukilinganisha katika kipindi kama hicho ambacho miradi iliyosajiliwa ilikuwa ya dola milioni 600,”alisema.
Rais Samia aliongeza kuwa mauzo ya bidhaa za nje yameongezeaka kufikia dola bilioni 3.4 kutoka dola bilioni 2.4 katika kipindi kama hicho cha mwaka jana.
KILIMO NA MIFUGO
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Rais Samia alieleza kuwa serikali imehakiki mashamba hekari 237,941.9, kupima afya ya udongo, kuendelea kujenga vihenge vya kuhifadhi chakula na kukarabati na kujenga skimu za umwagiliaji.
Aidha, alisema serikali imefanikiwa kudhibiti nzige waliovamia maeneo ya kaskazini mwa nchi na kutafuta masoko ya mazao katika nchi za Kenya, Sudan Kusini, China, India, Ukraine, Umoja wa Ulaya (EU) Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Saudi Arabia.
Alieleza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), zimepatiwa sh. bilioni 129 kununua mahindi kwa wakulima kwa bei ya sh. 500 kwa kilo kutoka sh. 300 waliyokuwa wakidhulumiwa na wanunuzi.
Ili kutatua changamoto ya uhaba wa mbolea nchini iliyosababishwa na Uviko-19, Rais samia alisema Kampuni ya Mbolea ya Intracom imeanza kujenga kiwanda cha mbolea mkoani Dodoma lengo likiwa kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na kwa uhakika.
Pia, alisema viwanda vipya sita vya kusindika maziwa vimekamilika pamoja na kituo cha ukuzaji viumbe vya baharini huku serikali ikitenga sh. bilioni 50 kuanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi.
SEKTA YA MADINI
Rais Samia alisema sekta ya madini ni miongoni mwa maeneo yaliyopiga hatua ambapo kuanzia Machi hadi Septemba, mwaka huu, leseni 5,126 za madini zilitolewa zikiwemo tatu za uchimbaji mkubwa ikilinganishwa 3,195 kwa mwaka jana.
Alisema kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya dhahabu kimezinduliwa mkoani Mwanza chenye uwezo wa kuchakata kilo 480 za dhahabu ambapo serikali imeondoa VAT kwa watakaoleta madini kuingiza nchini kuchakatwa katika kiwanda hicho.
UTALII
Akizungumzia sekta ya utalii, Rais Samia alisema idadi ya watalii imeongezeka nchini ambapo Machi hadi Septemba, mwaka huu watalii 464,913 waliingia nchini, hivyo kuna uwezekano mkubwa kuvuka idadi ya watalii laki sita waliokuja Tanzania mwaka jana.
Alisema kupitia kipindi cha Royal Tour alichorekodi kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii nchini, baada ya kipindi hicho kukamilika taifa linatarajia kupata ongezeko la watalii na wafanyabiashara kutembelea maeneo mbalimbali.
MIRADI MKUBWA
Rais Samia alisisitiza kuwa miradi yote makubwa nchini iliyoachwa na Hayati Dk. Magufuli inaendelea kutekelezwa vizuri.
Alisema mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam umefikia asilimia 93, Morogoro hadi Makutupora umefikia asilimia 70 huku kipande cha Mwanza hadi Isaka kikiwa kimetengewa sh. trilioni 1.3.
Alisema ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwara umefikia asilimia 58, ujenzi wa meli mpya Ziwa Victoria umefikia asilimia 80.1.
Alieleza kuwa mikataba mitano ya ukarabati wa meli ya Mv Umoja, ujenzi wa meli mpya ya kubeba mabehewa, meli mpya ya abiria na mizigo katika bahari ya Hindi na meli ya kubeba mafuta ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika, inaendelea ikiwa na thamani ya sh. bilioni 317.4.
SEKTA YA ANGA
Akizungumzia mafanikio katika sekta ya anga, Rais Samia alisema Septemba mwaka huu, serikali imetia saini mkataba wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato uliopo Dodoma huku upanuzi wa viwanja vingine vya Mtwara, Songea na Iringa ukiendelea.
Rais Samia alisema ndege tatu zilizonunuliwa na serikali zimekwishawasili na kufikisha idadi ya ndege kuwa 11, zilizonunuliwa na serikali.
“Serikali imesaini mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine tano ambazo ni Dremliner moja, Boeing mbili, ndege ya mizigo moja na ndege moja ya Bombardier,”alisisitiza huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
UJENZI WA BARABARA
Kuhusu ujenzi wa barabara, Rais Samia alisema mbali na ujenzi wa barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma, serikali itajenga barabara za njia nne upande wa kwenda Singida, Dar es Salaam, Iringa na Arusha.
Alisema ujenzi wa madaraja makubwa ya Wami, Selander, Kigongo Busisi unaendelea huku sh. bilioni 216 zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ukifanya matengenezo ya barabara za vijijini ambazo nyingi ziliharibiwa na mvua.
NISHATI
Kuhusu nishati alisema ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, umefikia asilimia 55.9 ambapo sh. bilioni 699 zimetumika kuanzia Aprili hadi Septemba, mwaka huu.
Alieleza kuwa sh. bilioni 112.9 zimetumika kujenga njia ya umeme kutoka katika bwawa hilo kwenda kwenye kituo kikuu cha umeme kilichopo Chalinze mkoani Pwani.
AFYA
Kwa upande wa afya, alieleza kuwa serikali imepokea dozi ya chanjo ya Uviko 19, milioni 1.5 kutoka Marekani na dozi milioni 1.6 kutoka COVAX na hadi juzi Watanzania 846,000 wamechanja chanjo hiyo.
Alisema serikali imejenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kujikinga na Uviko-19 kilichopo Dar es Salaam.
Rais Samia alieleza kuwa sh. bilioni 234 zimetumika kununua dawa, sh. bilioni 26.3 zimetumika kununua vifaa mbalimbali na sh. bilioni 7.9 zimetumika kununua mashine ya kupasua ubongo bila kupasua kichwa.
Aidha, alisema kupitia tozo ya miamala ya simu, serikali imetoa sh. bilioni 37.5 kujenga vituo vya afya katika tarafa 150.
SEKTA YA ELIMU
Akieleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu, Rais Samia alisema sh. bilioni 145.5 zimetumika ndani ya miezi sita kugharamia elimu bila malipo.
Kadhalika, alisema sh. bilioni 208.9 zimetumika kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na Mei, mwaka huu serikali imepata mkopo wa sh. bilioni 972 kuimarisha elimu ya juu.
Alieleza kuwa sh. bilioni 18 zitatumika kujenga Chuo kikubwa cha Ufundi Dodoma, sh. bilioni 120 zimetumika kuimarisha miundombinu ya shule za misingi na sekondari ambapo sh. bilioni saba fedha za tozo za simu zimetumika kujenga madarasa 560.
MIRADI YA MAJI
Rais Samia alisema miradi ya maji 328 yenye thamani sh. bilioni 109 imekamilika itakayowanufaisha wananchi milioni 2.3.
“Miradi iliyokwama kama wa Same- Mwanga, miezi sita ijayo tunakwenda kumaliza na mradi huo,”alisisitiza.
UTOAJI HAKI
Rais Samia alisema serikali imejitahidi kuimarisha mfumo wa utoaji haki na usimamizi wa sheria pamoja na ukarabati wa mahakama.
Aidha, alisema serikali imeimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya maridhiano, upatanshi, usuluhishi, haki za binaadamu na demokrasia.
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, upotevu wa mapato na ubadhirifu, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeokoa sh. bilioni 2.7 na kukamilisha uchunguzi wa majalada 302.
Vilevile, alisema serikali imeimarisha uhuru wa habari na wananchi kujieleza, ongezeko la nafasi za wanawake katika uongozi na kuwezesha nchi kupata heshima kuwa kinara wa haki za usawa wa kijinsia kiuchumi.
Pia, alisema watumishi wapya 29,900 wameajiriwa, watumishi 8,802 wamebadilishiwa kada ya utumishi huku sh. bilioni 55 zikitolewa kulipa madeni kwa watumishi.
Aidha, Rais Samia alisema serikali itaanza kutekeleza mradi wa kujenga masoko ya wajasiriamali wadogo maarufu kama machinga.
Rais Samia alisema serikali imeendelea kukuza uhusiano wa mataifa ya nje na taasisi za kimataifa huku ikilinda uhuru wa nchi.
Alisema Tanzania imeachangia askari 290 na dola 882,473 kuwezesha ushiriki wa kulinda amani katka jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.
Rais alisema serikali itatilia mkazo kwa Watanzania kupata ajira katika mashirika ya Umoja wa Mataifa (AU).
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA