RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaagiza viongozi wa dini kurudi katika mafundisho, kukaa na waumini ili wawe na hofu ya Mungu na kutojihusisha na vitendo vya mauji.
Pia amewaagiza viongozi wa kimila na machifu wa makabila mbalimbali nchini, kuzungumza na wananchi wao kuhusu vitendo vya mauaji kwa kuwa hakuna mila na desturi zinazotaka watu kuuana.
Akizungumza mkoani Kagera, Februari 22, 2022, katika Jubilee ya miaka 25 ya Askofu Severine Niwemugizi, Rais Samia alisema viongozi wa dini wana kazi kubwa ya kuwasisitiza kumjua Mungu kwa kuwa matukio ya mauji yanayotokea yanatokana na watu kujitenga katika imani za dini na kutokuwa na hofu ya Mungu.
“Nitoe wito kwa viongozi wa dini zote turudi tena katika mafundisho yetu, tuzungumze na watu kuhusiana na haya, lakini tukiacha viongozi wa dini, nizungumze na viongozi wa kimila na machifu wenzangu tuna kazi kubwa ya kufanya hapa kwa sababu nyinyi mna sehemu kubwa ya kuaminiwa na jamii, tuwaambie watu kuwa kinachotokea sicho tulichoamrishwa na mila na desturi zetu,”alisema.
Aidha, amewataka viongozi wa dini kutumia sauti zao kuonya na kufundisha wanapoona watu wanaishi maisha ambayo hayampendezi Mungu katika nyanja zote kijamii, kisiasa na kidini.
“Kwa pamoja tunalaani matukio ya mauaji, ukatili na ukiukwaji wa haki za watu, endeleeni kuonya na sisi kwa upande wetu serikali tutaendelea kutafuta suluhu ya maovu hayo, ikibidi hata kubadili sheria au kutunga sheria mpya,” alisema.
Rais Samia ameongeza lengo la serikali ni kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa dini kwa kuwa nchi haiongozwi na mtu mmoja na kufanya hivyo kutasaida kuwepo amani na utulivu nchini.
Aidha, Rais Samia amesema katika Wilaya ya Ngara, Kagera mwaka 2020 kulikuwa na matukio 22 ya mauaji, mwaka 2021 matukio 20 na mwaka 2020 matukio matatu ya watu kujiua na mwaka 2021 matukio mawili ya watu kujiua.
Amesema ripoti zinazoletwa na tume baada ya kutokea kwa mauaji zinakuja na majibu kuwa yanatokana na wivu wa mapenzi, kuwania mali na msongo wa mawazo, huku sababu kubwa inaonekana ni kutokuwa karibu na Mungu.
Rais Samia ameongeza kuwa, serikali itajipanga kutoa mafundisho kwa wanafunzi shuleni kupitia somo la uraia, ili kuwajenga watoto kutojihusisha na vitendo vya mauaji.
MADENI TAASISI ZA DINI
Kuhusu madeni ya taasisi za dini, amesema serikali itafanya utafiti kujua fedha zinazopatikana katika hospitali za dini zinatumikaje na baada ya kujua itaangalia kiasi gani kitolewe kuchangia serikali.
Rais Samia ameeleza kumekuwa na maombi kutoka madhehebu mbalimbali kutaka kusamehewa madeni ya kodi, ambapo alisema serikali itafanya utafiti na kuangalia gharama zinazotozwa.
Amesema serikali imefanya utafiti na kuona bei zinazotozwa katika huduma za afya kwa hospitali za dini na serikali hazipishani sana, hivyo wanapata faida na inatakiwa kupitia fedha hizo wachangie shughuli za serikali.
Aidha, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, kufuatilia ardhi inayodaiwa ya kanisa hilo, ambayo iliazimwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ambayo ipo mikononi mwa halmashauri.
MAJI
Rais Samia aliongeza katika mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetenga sh. milioni 793 za kuchimba visima na kujenga mtandao wa mabomba ili kusaidia upatikanaji wa maji Ngara ambapo tayari sh. milioni 100 zimeshatolewa.
“Sh. milioni 100 zimeshatolewa kwa uchimbaji wa kisima, nitamtaka Waziri wa Maji aje kukagua kama fedha iliyokuja inafanya kazi iliyokusudiwa na baada ya kukamilika mradi huo itasaidia kuwanufaisha wananchi 36,699 waishio Ngara Mjini,” alisema Rais Samia.
KUHUSU WAKULIMA
Aidha, Rais Samia alisema serikali itapeleka timu kuangalia changamoto za vyama vya ushirika zinazosababisha wakulima kununuliwa mazao yao kabla ya wakati.
Alisema serikali inaendelea kutafuta wawekezaji ili wakulima waone namna gani ya kuingia ubia ili wapate na mwekezaji anufaike.
Rais Samia alisema serikali itachimba madini ya Nikel kwa kuwekeana ubia na mwekezaji huku ikihakikisha uchimbaji huo unawanufaisha wananchi wa Ngara.
WAZIRI TAMISEMI
Kwa upande wake, Bashungwa, alimpongeza Rais Samia kutoa sh. bilioni 15 kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 116 katika mkoa huo.
Na IRENE MWASOMOLA