RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema bado kuna changamoto ya rushwa katika sekta ya Mahakama kwa wenye nacho, ili kuwanyima haki wasionacho, hivyo kusababisha malalamiko.
Aidha, amesema kabla ya sensa ya watu na makazi, mwaka huu, watahakikisha suala la uwekezaji katika mfumo wa TEHAMA na Postikodi linafanyiwa kazi, ili kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda na maboresho kuelelekea Mahakama mtandao.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dodoma Februari 2, 2022, wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini, kilichoambatana na kaulimbiu isemayo ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mtandao.
Rais Samia alisema pamoja na uwepo wa uwazi wa uwajibikaji kwa Mahakama nchini, bado yapo malalamiko ya baadhi ya wananchi kucheleweshewa haki na wakati mwingine kunyimwa kabisa haki zao.
“Yapo malalamiko mengi ya wananchi hususan katika masuala ya mirathi na hasa kutoka kwa wanawake wajane na migogoro ya ardhi inayowasilishwa kwetu serikalini ili kuomba msaada tuingilie kati uamuzi wa Mahakama zetu, ili wapate haki zao,” alisema.
Rais Samia alisema kwa bahati mbaya, serikali haina mamlaka ya kutoa haki bila kutegemea Mahakama zilizopewa jukumu hilo la kisheria, hivyo kusisitiza watendaji wa Mahakama wenye dhima ya utoaji haki kutoa haki bila kufungwa na masharti ya kiufundi.
“Na hapa masharti ya kiufundi, nina maana kwamba, mwananchi anapoleta kesi yake Mahakamani hajui chochote, hajui apite njia gani, anategemea wakili kwa wale wenye uwezo wa kuweka wakili, lakini kwa yule asiye na uwezo, tunasema serikali tuna wajibu wa kumpa wakili, lakini sidhani kama wote wanapata mawakili,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Anayedhulumu ana uwezo wa kuweka wakili kwa hiyo, mawakili wanatumia njia zao za kiufundi jinsi ya kukwepa vipengele na kumweka hatiani au kumyima haki mwenye haki.”.
Alibainisha kuwa, pamoja na matumizi ya vifungu vya sheria na ufundi Mahakamani, kikubwa mtoa haki anatakiwa kusikiliza nafsi yake kama anatenda haki kwa anachofanya au la.
“Katika kutoa uamuzi utu wa mtu nao utazamwe hususan unayemhukumu, lakini na wewe unayetoa hukumu, utu wako unakutumaje uchukue fedha umnyime haki mtu au umpe aliyetumia umahiri na ufundi wa kifungu kumyima haki mwenye haki,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alieleza kwamba, bado katika sekta ya Mahakama kuna changamoto ya utoaji rushwa katika ngazi za chini, kama si za juu huku akitaka suala hilo kufanyiwa kazi.
“Bado vijipesa vinatembea, inawezekana sio katika ngazi za juu, lakini huko ngazi za chini ambako vinasababisha mwenye haki anyimwe haki au kwa lugha rahisi niseme rushwa bado ipo ndani ya sekta ya Mahakama,” alisema.
Aliwaagiza mawaziri wa Wizara wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuhakikisha wanafunzi wanapewa ujuzi mpya ili kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda.
Aidha, alisema serikali itafanya uendelevu wa uwekezaji mkubwa katika TEHAMA ili kuwezesha kukamilika kwa Mahakama mtandao, ambapo aliahidi kufanyia kazi.
Kuhusu suala la uwekaji umeme vijijini, mahakama kupewa kipaumbele, Rais Samia aliahidi kuwa, mawaziri wa kisekta watafanya hivyo.
Kuhusu ukamilishwaji wa anwani za makazi na postikodi ili kuwezesha mhimili wa mahakama kutumia mtandao, aliahidi kulikamilisha kabla ya siku ya sensa ya watu na makazi kufika.
Pia, alipongeza jitihada za Mahakama kuanza matumizi ya mfumo wa uundaji wa roboti/ akili bandia wa kutafsiri na kuandika taarifa za mashauri ya Mahakamani katika lugha zaidi ya 10.
Akijibu ombi la kuzindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama linalojengwa jijini humo pindi litakapokamilika, Rais Samia alitaka thamani ya matumizi ya fedha, ionekane na liwe la kueleweka si bora jengo.
“Tunajiandaa kuja kulifungua likikamilika, lakini ombi langu ‘value for money’ na kujenga kitu kinachoeleweka, vinginevyo nitakuja kukagua kabla ya kuzindua, nikiona mambo yamekwenda sivyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama tutaelewana,” alisema
Wakati huo huo, Rais Samia alikipongeza Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kubadilika na kuendana na lengo la kuundwa kwake huku akiahidi serikali itashirikiana nacho.
“Rais wa TLS, niwapongeze kwa kujitambua na kuelekea kwenye lengo la kuundwa kwenu, lakini hapa katikati, nadhani mnakumbuka na mnajua mlichokuwa mnafanya na kwa maana hiyo, serikali ipo pamoja nanyi na tutakwenda pamoja,” alisema.
NA SELINA MATHEW, DODOMA