MWANASIASA nguli nchini, Balozi Amina Ali, ameutaja mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani, kuwa nchi imefunguka kwa mafanikio.
Mwanasiasa huyo aliyeshika nafasi ya pili katika mchujo wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kuwania urais mwaka 2015, amesema Rais Samia amelifanya taifa kuwa na nguvu na kuthaminika duniani kutokana na kufungua milango ya kidiplomasia na kiuchumi.
Balozi huyo wa zamani wa Umoja wa Afrika, amewataka wananchi kudharau wanasiasa uchwara wanaotafuta hila, kwa sababu ukweli unaonekana kuwa mwaka mmoja wa uongozi ametosha katika nafasi ya mrithi wake Hayati Dk. John Magufuli baada ya kuendeleza miradi ya kimkakati.
Amesisitiza kuwa Rais Samia amefiti na ni jahazi lisiloyumbishwa na mawimbi, kwa kuwa amesimama kidete katika kuhakikisha maendeleo ya sekta madini, afya, elimu, uchumi, siasa na jinsia yanafikiwa ipasavyo.
DIPLOMASIA
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Balozi Amina amesema, katika kipindi hicho Rais Samia amefanya vizuri katika kila sekta na kuifungua nchi katika diplomasia hatua iliyolijengea heshima taifa.
“Kuanzia alivyounda Wizara ya Mambo ya Nje tuliona mwelekeo wake katika kuijenga Tanzania yenye nguvu na kuipandisha hadhi ndani ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla,” alisema.
Amesema Rais Samia amerejesha idara zote muhimu katika wizara hiyo, ikiwemo ya diplomsia na uchumi ambayo mkurugenzi wake alikuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Balozi Edwin Rutageruka, aliyefariki hivi karibuni.
Alisema utendaji wake umefunguka na kumgusa kila mtu hatua iliyoweka picha ulimwenguni kuwa Rais mwanamke wa mfano, anayewafanya Watanzania kutembea kifua mbele.
“Sisi mabalozi ni mashuhuda wa hilo, hatuoni haya kujitambulisha kwa wenzatu huko duniani kuwa tunatoka Tanzania inayoongozwa na Rais Samia,”alisema.
Balozi Amina alisisitiza kuwa Rais Samia amemaliza kiu ya wengi katika masuala ya diplomasia na uchumi shirikishi.
UCHUMI
Akizungumzia maendeleo ya kiuchumi alisema uongozi wa Rais Samia umeonyesha mwelekeo wa sekta hiyo na kufungua uchumi wa nchi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Makusanyo yameongezeka kwa kuwa Tanzania ina utulivu wa maamuzi na umakini katika kusimamia uchumi ukweli tuna picha halisi ya Tanzania ijayo ya mbele ambayo ni ya uchumi si wa kufikirika ila unaoonekana kwa kila mtu,”alisema.
Alisema ni Rais anayejua tulipotoka, tulipo na tunapotakiwa kwenda hatua iliyomlazimu kuhakikisha miradi yote ya kimkakati hususani iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dk. Magufuli anaiendeleza ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama madaraja, barabara vitega uchumi muhimu kama Bwawa la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa
UWEKEZAJI
Mwanasiasa huyo alieleza kuwa sekta ya uwekezaji sasa imekua na wawekezaji wengi zaidi wamejitokeza.
Alisema safari zake za nje zimepunguza vikwazo, kuondoa kero zisizo za lazima na kusimamia ipasavyo utendaji kwa kudhibiti urasimu zimewavuta wawekezaji wengi kuja nchini.
“Sekta ya uwekezaji imekua inaonekana anawafuata wawekezaji huko huko nchini mwao, anafanaya nao mazungumza akiwa na timu ya wataalamu na wanaona fursa zilizopo wanakuja huyu ndiyo Rais Samia,”alisema.
BIASHARA
Alisema sekta ya biashara imekua na kufungua fursa za masoko ndani na nje ya nchi.
Balozi AMina alisisitiza kuwa kwa sasa bidhaa za Tanzania zina soko kubwa nje ya nchi ikiwemo la kahawa, mboga, viungo na rasirimali bahari wakiwemo dagaa ambao wana soko kubwa mjini Lumbumbashi nchini DRC Congo.
SIASA
“Mbali na hayo amekuwa ni kiongozi anayeonyesha kwa vitendo nidhamu ya hali ya juu kwa waasisi wetu na viongozi waliomtangulia kwa kusifu mazuri waliyofanya na kuayaendeleza,”alisema.
Alieleza kuwa mwaka mmoja wa Rais Samia amekijengea Chama heshima ndani na nje ya nchi na hotuba yake katika ufunguzi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere juzi mkoani Pwani wilayani Kibaha, imejipapanua namna Chama kitakavyojikita katika kuwandaa viongozi walio na maadili, weledi na utumishi wenye nidhamu kwa kuwa na elimu ya Itikadi.
ELIMU
Alisema uongozi wa Rais Samia katika mwaka mmoja wa utendaji wake, umejionyesha alivyogusa sekta zote muhimu ikiwemo ya elimu ambapo ameendelea hatua ya elimu bure kuweka mazingira rafiki ya kusomea na kujali mahitaji ya walimu na watendaji wengine.
“Pia amefungua milango ya Watanzania kupata fursa ya masomo na kubadilishana uzoefu kutoka nchi nyingine duniani,”alisema.
JINSIA
Akizungumzia maendeleo sekta ya jinsia Balozi Amina alisema Rais Samia ni mwanamke wa pekee ambaye kama ni jahazi limetulia, kwakuwa ametambua thamani ya mwanamke bila wivu wala choyo amedhamiria kuwashika mkono na kuwainua.
Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe nchini, Gertrude Mongella, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia jambo la kujivunia ni kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini.
Alieleza mkuu huyo wa nchi ameiongoza nchi kufuata misingi iliyoasisiwa na waasisi wa taifa ndiyo sababu ya kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu.
“Naomba niongee kwa sentensi moja kwamba, moja ya jambo tunalojivunia katika mwaka mmoja wa serikali hii ni kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu na kazi inaendelea,” alieleza kwa ufupi.
Naye, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Ave Maria Semakafu, alisema Rais Samia ameandika historia katika kipindi hicho.
“Ameandika historia kwani ni mara ya kwanza tunapata kiongozi wa juu mwenye jinsia tofauti, Rais Samia amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais hilo ni jambo kubwa kwetu,” alisema.
Alisema pia Watanzania wanapaswa kujivunia juhudi za kiongozi huyo za kuhakikisha anatekeleza haki na usawa katika fursa zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alibainisha jambo jingine katika kipindi hicho ni kufanikisha kupatikana kwa Waziri wa Ulinzi wa kwanza mwanamke Dk. Stergomena Tax, jambo lililowashangaza wengi.
Dk. Semakafu ambaye pia ni mwanaharakati wa jinsia, alifafanua matendo ya Rais Samia katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake yameendelea kuithibitishia jamii kwamba mwanamke anastahili haki zote kama ilivyo wanaume.
“Utaona kwa sasa tuna wanawake wengi katika Baraza la Mawaziri hii inatokana na hatua yake ya kuwapa fursa wanawake, tumeona katika teuzi nyingi anazozifanya anazingatia usawa wa jinsia,” aliongeza.
Dk. Semakafu ambaye ni Mratibu wa Jumuiya ya wanawake wenye itikadi tofauti za kisiasa (TWCP-Ulingo), alisisitiza mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia umeonyesha dalili njema katika maridhiano ya kisiasa ambapo, aliagiza kuundwa tume ya kushughulikia changamoto zinazosababisha maelewano duni baina ya vyama vya siasa.
Aliongeza kwamba Rais Samia ameendelea kuonyesha uhalali wa mwanamke kupewa uongozi kwani wana sifa zote yaani uwezo na akili.
Alitaja jambo lingine la kujivunia ni uamuzi wake wa kuyaimarisha majukwaa ya wanawake aliyoyaasisi, akisema hayo yatawatoa wanawake kutoka kufanya biashara ndogondogo na kuwaingiza kushiriki katika uchumi wa viwanda.
Hatua hiyo inafikiwa ikiwa Rais Samia anatarajia kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake Ifikapo Machi 19 mwaka huu.
Aidha katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, Rais Samia ameonyesha mwelekeo wa siasa za urafiki, baada ya kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo Tundu Lissu.
Pia, katika kipindi hicho ameiingiza Tanzania katika ramani ya dunia kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali, hivyo kuleta tija ya misaada na mikopo ya masharti nafuu.
Rais Samia ndani ya kipindi hicho amefanya ziara kadhaa katika mataifa mbalimbali likiwemo la Kenya na kusababisha kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara vilivyokuwepo baina ya mataifa hayo.
Pia, ziara yake ya kwenda Ulaya imerudisha uhusiano baina ya Umoja wa Ulaya (EU) na Tanzania na hivyo kuwezesha misaada iliyokuwa ikitolewa na jumuiya hiyo kuendelea kutolewa ukiwemo wa ujenzi wa viwanja vya ndege.
Katika uwajibikaji ndani ya serikali, Rais Samia ndani ya mwaka mmoja ameonyesha uwazi, uzalendo na uchungu na fedha za umma, hilo limejidhihirisha wakati wa matumizi ya fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuleta ustawi na kukabili Uviko-19.
Kuhusu usawa wa jinsia, Rais Samia amekuwa akilitekeleza hilo kwa kuzingatia jinsia zote katika teuzi alizozifanya na kuvunja rekodi ya baadhi ya nafasi kuwapa wanawake ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa Tanzania.
Mariam Mziwanda Na Juma Issihaka