RAIS Samia Suluhu Hassan, amuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, kutoa Sh. bilioni moja kabla ya Novemba 30, mwaka huu, kwa ajili ya kuchangia ujenzi unaoendelea wa hospitali ya Wilaya ya Arusha.
Aidha, amekabidhi hundi ya Sh. bilioni 1.39 kwa vikundi 152 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Rais Samia alitoa agizo hilo Oktoba 17, 2021, baada ya kuzindua hosptali hiyo ya kisasa ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh. bilioni 2.5 ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
“Nimefurahishwa sana kwa jinsi ambavyo mmekusanya vizuri mapato yenu ya ndani na kujenga hospitali hii ya kisasa. Kwa sababu hii, nimemwagiza waziri wa TAMISEMI, Ummy, kuleta hapa kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi huu ambao tayari wana majengo mawili ya kisasa yaliyokamailika,” alisema.
Rais Samia alisema licha ya kutoa fedha hizo, pia serikali kuu itatoa dawa na vifaatiba katika hospitali hiyo, ili wanachi waendelee kupata huduma bora za afya.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwaomba wananchi kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya Jiji la Arusha na maendeleo yao, huku akiwataka watumishi kuendelea kukusanya mapato ya jiji hilo kwa uadilifu.
Kwa upande wake, Waziri Ummy alimshukuru Rais Samia kwa kufungua hospitali hiyo na kuahidi kuzitoa fedha hizo kabla ya Juni 30, mwaka huu kama alivyoagiza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk. John Pima, aliishukuru serikali kwa kuwapatia fedha hizo ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ambayo moja ya majengo yake litakuwa na uwanja mdogo wa ndege ili ndege ndogo zinazoleta wagonjwa hosptalini hapo zitue bila adha ya shida.
Wakati huo huo, Rais Samia alisema serikali inafanya utaratibu wa kuwalipa stahiki zao waliokuwa wafanyakzi wa shamba la maua lililokuwa linamilikiwa na kampuni ya Kiliflora Ltd, ambalo mwekezaji wake Jerry Goh ameshindwa kuendeleza mashamba hayo.
Alisema hivi sasa serikali iko katika hatua ya kuuza mali zilizoachwa na mwekezaji huyo kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya stahiki hizo ikiwemo mishahara na makato ya NSSF.
“Ninajua kuna wafanyakazi hapa zaidi ya 1,000 ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye mashamba hayo na kuna mahali mwekezaji alikosea akashindwa kulipa stahiki zenu. Naomba niwaondoe hofu mtalipwa haki zenu zote zikiwemo za NSSF,” alisema.
Rais Samia aliyazungumza hayo baada ya kukagua mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 520 katika eneo la Chekwreni, wilayani Arumeru.
Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, alisema CCM itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Na LILIAN JOEL, Arusha