JARIDA maarufu duniani la ‘TIME 100,’ limemtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.
Katika orodha hiyo, Rais Samia Rais Samia ameungana na marais kama Volodymir Zelenskyy wa Ukraine, Xi Jinping wa China, Vladimir Putini wa Russia na Joe Biden wa Marekani.
Viongozi wengine mashuhuri waliojumuishwa katika orodha hiyo ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, Makamu Waziri Mkuu wa China, Sun Chunlai na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa jerumani, Ursula von der Leyen,
Rais Samia ametajwa katika orodha hiyo kufuatia uongozi wake tangu alipoingia madarakani Machi mwaka jana, kuwa wenye kusisimua hususan kuanzisha mazungumzo kati ya viongozi wa vyama vya wapinzani na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa jarida hilo maarufu, Rais Samia amechukua hatua hiyo kwa lengo la kujenga upya imani katika mfumo wa kidemokrasia na kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wengi duniani.
RAIS MSTAAFU LIBERIA AMZUNGUMZIA
Akimzungumzia Rais Samia kupitia jarida hilo, Rais mstaafu wa Liberia, Hellen Johnson Sirleaf, alisema Rais Samia wakati akiingia madarakani Machi 2021, uongozi wake ulikuwa katika nyakati ngumu.
Alisema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia mlango wa majadiliano kati ya mahasimu wa kisiasa ulifunguliwa, hatua mbalimbali zimechukuliwa kujenga imani katika mfumo wa demokrasia, kuongeza uhuru wa habari, hivyo wanawake na wasichana wana mtu wa mfano.
“Septemba 2021, ikiwa ni miezi michache tangu aingie madarakani, Samia alitoa hotuba yenye muelekeo kama kiongozi wa awamu ya sita mwanamke wa Afrika, alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” alieleza kiongozi huyo ambaye ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel ambaye pia ni Rais wa kwanza Afrika kuchaguliwa kidemokrasia.
Alisema Rais Samia alisimama katika eneo alilowahi kusimama yeye miaka 15 iliyopita akiwa mwanamke wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia Afrika.
“Kama mwanamke wa kwanza Rais katika historia ya nchi yangu, mzigo wa matarajio ya kufanikisha usawa wa kijisia ni mzito mabegani mwangu. Alipokuwa akizungumza maneno hayo mazito, sikuweza kumsaidia lakini nilifikiria jinsi mabega yenye nguvu waliyonayo wanawake viongozi na namna wanavyoweza kuleta mabadiliko,” Hellen alimueleza Rais Samia.
NA MUSSA YUSUPH