BENKI ya Dunia (WB), imetangaza kupungua kwa kiwango cha umasikini nchini kutoka asilimia 27.1 mwaka 2020 hadi asilimia 27.0 mwaka 2021, huku ikipongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kuondoa matabaka ya jinsia katika fursa za maendeleo ambazo ni siasa, uchumi na jamii.
Huo ni mwendelezo wa mafanikio ya Rais Samia, ambapo tayari amekuwa akitajwa kuweka mazingira mazuri ya kisera katika biashara, kuimarisha diplomasia ya uchumi na mapambano ya kisayansi dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19.
Mwenendo huo wa hali ya umasikini ilitolewa na Mkurugenzi wa WB kwa nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Dk. Mara Warwick, wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya 17 ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania, yenye kaulimbiu ya ‘Uwezeshaji wanawake: Kupanua ufikiaji wa rasilimali na fursa za uchumi’.
Dk.Mara alieleza hatua hiyo ni matokeo ya juhudi zilizochukuliwa katika kukabiliana na janga la Uviko-19,ikiwemo ya mpango wa chanjo kwa wananchi ambao umesababisha shughuli za uchumi kuendelea kuimarika nchini.
MWELEKEO WA GDP
Kuhusu mwelekeo wa ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), Dk. Mara alisema sekta ya malazi na migahawa, madini na umeme zilichangia kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa pato hilo, kwa robo mwaka katika robo ya tatu ya mwaka jana.
Kwa mujibu wa Dk. Mara, juhudi nyingine zilizofanywa ni maboresho katika uzalishaji wa saruji, umeme, mikopo ya sekta binafsi, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, uagizaji wa bidhaa zisizo za mafuta kutoka nje, mawasiliano ya simu, uhamaji na kuwasili kwa watalii.
“Kwa sababu ya maendeleo haya chanya, Benki ya Dunia inakadiria kiwango halisi cha ukuaji wa Pato la Taifa cha asilimia 4.3 na kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa cha asilimia 1.3 mwaka 2021, kufuatia kupungua kwa Pato la Taifa kwa asilimia 1.0 mwaka 2020,” alisema.
VITA DHIDI YA UVIKO
Aliishauri serikali kuimarisha mwitikio wake katika janga la Uviko-19, katika muda mfupi kwa kushirikiana na sekta binafsi katika muda wa kati hadi mrefu.
Aidha, Dk. Mara alifafanua kwamba hatari kwa mtazamo wa kiuchumi wa Tanzania zimepungua, lakini hilo litaimarika zaidi iwapo sekta binafsi itashirikishwa vyema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkazi wa WB, mpango wa utoaji chanjo ya Covid-19 kwa wananchi umechochea kuongezeka kwa biashara, ushirikiano wa kikanda na mageuzi ya sera iliyoundwa kuboresha mazingira ya biashara na kusaidia ukuaji wa sekta ya binafsi.
Dk. Mara alisisitiza kuna umuhimu wa serikali kuimarisha juhudi katika kukabiliana na janga la Uviko-19, ili kuwezesha kuondolewa kwa vikwazo vya usafiri katika baadhi ya nchi na hatimaye sekta ya utalii kuimarika zaidi.
Aliongeza kwamba, taarifa hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuongeza upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji mali.
USAWA WA KIJINSIA
“Sasa ni wakati wa Tanzania kuchukua hatua, Rais Samia Suluhu Hassan, ameweka dira ya kimkakati yenye matarajio ya mbele kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa Tanzania. Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 pia inasisitiza usawa wa kijinsia katika nyanja zake za kijamii, kiuchumi na kisiasa,”alisema.
Alieleza kwa Tanzania ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi umeongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2000, hadi asilimia 80 mwaka 2019, juu ya wastani wa asilimia 63 kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA).
Dk. Mara alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali lakini bado, wanawake nchini wanakumbwa na vikwazo hasa katika upatikanaji wa ardhi na rasilimali, jambo ambalo linaathiri tija yao katika uchumi.
Alibainisha kwamba asilimia 25 ya wanaume nchini ndiyo wamiliki pekee wa ardhi, ikilinganishwa na asilimia nane ya wanawake, huku makadirio yakionyesha asilimia 42 ya wanawake nchini ndiyo wenye uwezo wa kuzifikia akaunti za benki, wakati wanaume ni asilimia 52.
“Inakadiriwa kuwa asilimia 22 ya wanawake wa Tanzania wanajishughulisha na ajira za ujira, ikilinganishwa na asilimia 48 ya wanaume. Kati ya wafanyakazi wanaolipwa mishahara wanawake hupata senti 88 pekee kwa kila dola inayopatikana kwa wanaume,” alisema.
Alisema hata katika sekta ya kilimo uzalishaji wa wanawake ni kati ya asilimia 20 na 30 tu, kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kifamilia, kukosa zana za kilimo na pembejeo.
“Makadirio yanaonyesha kuwa kuziba pengo la kijinsia la masharti katika tija ya kilimo kunaweza kuwainua takriban Watanzania 80,000 kutoka katika umaskini kila mwaka huku kukiongeza pato la kilimo kwa mwaka kwa asilimia 2.7 na kukuza Pato la Taifa kwa asilimia 0.86,” alisema.
Ili kuimarisha uwezo wa wanawake, Dk. Mara alisema taarifa hiyo inapendekeza waboreshewe ujuzi kupitia fursa zilizopanuliwa za uanagenzi na programu za mafunzo.
Alitaja nyingine ni kuimarisha haki za ardhi za wanawake kwa kutoa ruzuku ya hati miliki ya ardhi kwa kaya na motisha ili kuwahimiza wanandoa kumiliki ardhi pamoja, kupanua uwezo wa wanawake kutumia pembejeo za kilimo, teknolojia za kidijitali ili kuboresha uzalishaji wa kilimo kwao.
Pia, alisema wanawake waimarishiwe uwezo wa kusimamia fedha zao za kibinafsi na za biashara, kukomesha ndoa za watoto, na kutoa usaidizi wa malezi ya watoto ili kuruhusu na kuhimiza ushiriki mkubwa wa wanawake katika nguvu kazi.
“Jambo jingine ni kutekeleza sheria zinazowalinda wanawake dhidi ya ukatili,” alisema.
Ripoti hiyo ni ya 17 kutolewa ambapo hutolewa kila baada ya miaka miwili, ikiangalia mambo mbalimbali, ambapo ripoti ya 16 iliangalia mageuzi ya kimfumo katika sekta ya utalii, ili iwe endelevu.
NA JUMA ISSIHAKA