RAIS Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa Machinga nchini, zikiwemo za serikali kuwatambua rasmi kama kundi maalumu na kuahidi kujenga masoko ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini.
Orodha ya neema hizo ni pamoja na kuwaboreshea vitambulisho, kuwaongezea fedha katika Sacoss, kuwajengea masoko makubwa, kuanzishwa kwa madawati ya sera zinazowasimamia katika wilaya na kujenga masoko pembezoni mwa mji.
Rais Samia ametangaza neema hizo Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na viongozi wa Machinga.
Katika orodha hiyo ya neema, pia Rais Samia amezielekeza benki kuja na programu maalumu zitakazosaidia wanawake, vijana na makundi ya Machinga kukopa kwa njia nafuu na kukuza mitaji yao.
Rais ameahidi kuzungumza na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili kufahamu mipango ya matumizi ya fedha za Uviko-19 sh. bilioni tano, ili kuona ni namna gani zinaweza kuongeza nguvu katika kutunisha mtaji wa fedha wa Saccos ya Machinga.
“Nimewaelekeza benki waje na programu maalumu zitakazosaidia wanawake au vijana, kupitia programu hizo makundi ya Machinga kwa madaraja yao tutaangalia jinsi mtakavyokopa kwenye benki, kwa njia nafuu sana kwa ile mipango watakayokuja nayo,” amesema.
VITAMBULISHO VYA MACHINGA
Akizungumzia vitambulisho vya Machinga, Rais Samia alisema baada ya Sensa ya Watu na Makazi serikali itakuja na vitambulisho maalumu vya Machinga vitakavyokuwa na taarifa muhimu na kusomeka katika mashine.
Akijibu risala ya Machinga walioomba ujenzi wa masoko makubwa, Rais Samia alisema serikali itakaa na wafanyabiashara wenye uwezo wa kujenga masoko hayo na kuangalia mifumo na viwango rafiki watakavyotozwa Machinga.
Aidha, Rais Samia alisema kupitia Wizara ya Kazi, Kazi, Ajira na Vijana, wataandaa Madawati ya Sera katika Wilaya yatakayosimamia Machinga.
“Kutakuwa na madawati mbalimbali ya sera katika Wilaya nitaongea na TAMISEMI na Wizara ya Biashaara wakae waone, lakini Wizara nzuri ambayo kundi lenu litaingia huko ni Wizara ya Vijana na Kazi kule sasa tutataka sera iandikwe huko,” alisema.
MASOKO PEMBEZONI MWA MIJI
Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fungu maalumu katika bajeti zao, ili kufanya maboresho katika maeneo ambayo Machinga wanafanyia kazi.
Rais alisisitiza mpango wa serikali kujenga masoko yenye hadhi ya juu katika wilaya na maeneo ya pembezoni mwa mji, ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wasilazimike kwenda katikati ya mji.
“Tunajitahidi kutafuta maeneo mengine ya wazi kwa ajili ya kujenga masoko, kule katika wilaya ili watu wote wasimiminike katikati ya mji, maeneo yenyewe ni masoko ya hadhi ya juu, serikali tunajitahidi kutafuta fedha ziwe za ndani hata kama tutakopa tutakusanya fedha katika masoko tutarudisha,” alisema.
Aidha, aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), kuruhusu mabasi kufika katika maeneo yenye masoko.
Aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusimamia vizuri uondoaji wa Machinga barabarani na kuwapangia utaratibu maalumu.
AWAPONGEZA MACHINGA
Mkuu wa nchi aliwapongeza Machinga kwa kuanzisha vyombo vyake vya habari, likiwemo gazeti huku akitaka wapewe mafunzo na semina kutoka Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari, juu ya namna bora ya kuendesha vyombo hivyo kwa kufuata sheria .
Aidha, Rais Samia aliwataka Machinga kutokutumiwa na wafanyabiashara ili kukwepa kulipa kodi kwani kufanya hivyo kunaikosesha serikali mapato.
SUALA LA MOTO
Kuhusu ajali za moto katika masoko, Rais Samia aliwataka wafanyabiashara hao kujisimamia huku akisema baadhi ya matukio hayo hutokana na sababu mbalimbali.
“Ndugu zangu tumekua, sasa tunatakiwa kujisimamia. Lilipoungua Soko la Kariakoo tuliambiwa ni umeme, hasara ikapatikana watu ikabidi kuondoka ,imeungua Karume tumeambiwa mishumaa lakini, hata moto unapotokea hakuna maeneo ya kupita na magari kuzima moto,”alitoa angalizo Rais.
Aliahidi kuandaa mafunzo yatakayotolewa mara kwa mara kwa Machinga.
VITA YA UVIKO-19
Rais alisisitiza umuhimu wa Machinga kuchukua hadhari ya Uviko-19 na kuwataka viongozi wa mikoa kusimamia utoaji chanjo.
Gazeti hili lilifika katika soko la Mchikichini na kujionea ujenzi wa vizimba na urekebishaji wa njia ukiendelea.
Katika hatua nyingine, Ofisa Tarafa wa Kata ya Kariakoo, Christina Kalekezi, alisema kabla wafanyabiashara kuanza ujenzi wa vibanda vya biashara atahakikisha njia inatengenezwa ili kuweka miundombinu mizuri ya kupita.
Alisema kazi hiyo imeanza jana na atahakikisha magari yanayopeleka bidhaa katika soko hayapati shida kuingia.
Katika upanuaji wa njia hiyo, alisema kuna baadhi ya maeneo yatapunguzwa na mengine kuondolewa na wafanyabiashara watakaoathirika watafuata utaratibu kupewa maeneo mengine.
“Mfanyabiashara atakayekosa eneo la kufanyiabiashara kwa sababu ya kupunguzwa ili kupata njia, afike katika ofisi zetu ili tumfanyie utaratibu utakaokuwepo,’’ alifafanuan Christina.
MKUU WA MKOA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Malla,aliomba maeneo ya Mashirika ya nyumba ya Tifa (NHC) nay ale ya DDC yabadilishwe na kuwa masoko, ili yawasaidie wafanyabishara hao.
LUSINDE
Naye Makamu Mwenyekiti wa Mchinga Taifa, Steven Lusinde, alimpongeza Rais Samia kwa kuamua kuwapanga upya wafanyabishara hao kwa kuondoka barabarani na kuwapeleka katika masoko maalumu.
IRENE MWASOMOLA Na Rehema Maigala