NA MARIAM MZIWANDA
SERIKALI imetoa sh. bilioni 123, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha dawa za vidonge, ili kuondoa uhaba uliopo nchini na kupunguza bajeti ya manunuzi kutoka nje ya nchi.
Imeelezwa kiwanda hicho kitajengwa Mkoani Njombe, ambapo kitakuwa na uwezo wa kuzalisha dawa kwa siku mbili mfululizo.
Akizungumzia hatua hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Godwin Mollel, amesema fedha hizo zimetolewa nje ya bajeti ya mwaka huu.
“Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa nchini, kitachosaidia kuboresha huduma za afya, kuongeza upatikanaji wa dawa na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kununua nje ya nchi,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesisitiza, kiwanda hicho kinajengwa Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge na kushusha gharama za bei, hususani kwa vidonge vilivyokuwa vinanunuliwa nje.
“Pia kitaongeza uwezo kwa dawa ambazo zilikuwa zinanunuliwa mara moja, sasa zitanunuliwa mara mbili mpaka mara tatu,”amesema Dk. Mollel.
Kadhalika, ameongeza kuwa, hatua hiyo itaimarisha hali ya huduma za afya na kuendelea kuwa bora nchini hususan katika upatikanaji wa dawa, huku serikali ikiendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa ili kukabiliana na uhaba uliokuwepo.
Amesema hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni muda mfupi wa uongozi wa Rais Samia na fedha hizo zilizotoka kabla ya bajeti mpya, zimelenga kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwa, serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kukosekana kwa dawa na tayari Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, amepokea mrejesho kutoka kwa timu ya ukaguzi aliyounda kwenda katika hospitali za mikoa kufanya uchunguzi wa tatizo hilo.
“Na utekelezaji wake wa matokeo hayo unaanza kufanyiwa kazi, ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa nchini,” amesema.
Dk. Mollel, amesema serikali inaendelea kumalizia mchakato wa bima ya afya kwa wote, utakaosaidia kila mwananchi kupata huduma bora.
Katika hatua nyingine, amesema kupitishwa kwa bajeti itakayokidhi mahitaji ya kuboresha sekta hiyo na sekta zote ambazo kwa kiasi kikubwa zina akisi masuala ya afya, itasaidia kuwepo kwa mazingira bora ya maisha ya wananchi.