MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Rashid Chuachua, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa zaidi ya sh. bilioni 5.81 kuboresha sekta ya elimu katika wilaya hiyo yenye Halmashauri mbili.
Amesema fedha hizo zitatumika kujenga madarasa.
Dk. Chuachua aliyasema hayo alipozungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Tulia Street Talent Competition, uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, jijini Mbeya.
“Rais Samia ameendelea kutoa fedha za elimu bure, ambapo zaidi ya sh.bilioni 1.8 zimepelekwa katika shule zetu, kwa hiyo anaendelea kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania,” alisema.
Kuhusu chanjo ya Uviko-19, Dk. Chuachua aliwapongeza wananchi zaidi ya 20,000 waliopatiwa chanjo wilayani humo.
Aliongeza kuwa wamepokea chanjo nyingine aina ya Sinovac, ambayo inaendelea kutolewa kwa wananchi ili kulinda afya zao, kwa kuwa chanjo ni jambo la muhimu.
“Siku ya kwanza tulipozindua chanjo aina ya Sinovac, zaidi ya wananchi 600 walichanjwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Chuachua, Halmashauri ya Wilaya Mbeya zimepelekwa chanjo dozi 4,500, ambazo mpaka sasa tayari wananchi 2,000 wameishapata huduma hiyo, ndani ya siku nne.
Aliwataka wananchi ambao hawajachukua uamuzi wa kuchanja, ni vema wakachanja ili kulinda afya zao.
NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA