RAIS Samia Suluhu Hassan, amevutiwa na utendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kuongeza alama tano za barabarani kwa ajili ya walemavu.
Hatua hiyo ya TANROADS imefikisha alama 183 za barabarani, tofauti na awali walipokuwa na alama 178.
Aidha, amewaagiza watendaji wa TANROADS kote nchini, kuboresha michoro ya watembea kwa miguu na waendesha baiskeli katika barabara mpya zitakazojengwa na serikali.
Akizungumza katika banda la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa, mkoani Arusha, Rais Samia alisema ujenzi mpya wa barabara unapaswa kuwa na mfumo huo ili kuepusha ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikipoteza uhai wa Watanzania wengi.
“Nawapongeza kwa mchoro huu mzuri wa mfumo mpya wa kuanza kujenga barabara zetu, lakini wekeni michoro vizuri kwa ajili ya watembea kwa miguu na waendesha baiskeli kwa ajili za kupunguza ajali za barabarani,” alisema.
Pia aliipongeza TANROADS kwa hatua ya kuongeza mfumo wa alama kwa wenye ulemavu wa macho, viungo na ulemavu wa ngozi.
Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, alisema TANROADS imekuwa ikitoa elimu ya mara kwa mara kwa watumiaji wa barabara ili kuhakikisha hali ya usalama wa barabara inaimarika kila wakati.
Alisema TANROADS wana mizani 64 katika maeneo ya kimkakati kwa ajili ya kupima uzito na wamefunga mfumo wa kamera za kisasa za usalama (CCTV) katika mizani 13 ya majaribio kudhibiti mianya ya rushwa.
“Mfumo huu wa CCTV kamera tunarajia ulete mafanikio chanya ambapo mfanyabiashara akilipa faini yake kwenye moja ya mizani maofisa wote walioko katika ofisi za TANRONDS katika maeneo mbalimbali nchini wanaona faini hiyo moja kwa moja”.
Alisema kutokana na sheria ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya mwaka 2016 ya kutaka usajili wa mizigo mipana na mizito kuombewa kibali kwa njia ya mtandao, wameitekeleza na usajili huo unafanywa na mfanyabiashara yeyote akiwa ndani au nje ya nchi mwanachama wa EAC.
“Kwa sasa tunatoa vibali vya mizigo ya aina hiyo kwa njia ya mtandao, ambapo mtu anaomba na kulipa moja kwa moja na kupata kibali siku hiyo hiyo na tunafanya kazi ya utoaji wa vibali kwa saa 24,” alisema.
Mhandisi Mativila alisema kabla ya uwepo wa mfumo huo, walikuwa wanatoa vibali 60 hadi 100 kwa siku na sasa wanatoa vibali 200 hadi 400 hatua ambayo imeiongezea serikali mapato na kupunguza foleni katika mizani.
Na LILIAN JOEL, Arusha