RAIS Samia Suluhu Hassan, amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuwekeza Tanzania kwa kuwa, serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuimarisha mazingira ya kibiashara.
Akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ufaransa, jijini Paris Ufaransa, Februari 14, 2022, Rais Samia aliwaalika wadau hao wa biashara kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania ikiwemo ya sekta ya mifugo, kilimo, madini na nyinginezo.
“Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya kisheria na kikatiba katika sekta ya umma, ili kuhakikisha kunakuwepo na maziringa mazuri ya kuanzisha na kufanya biashara nchini,” alisema.

Rais Samia amesema hatua mbalimbali zilizochukuliwa na uongozi wake kuimarisha mazingira ya biashara, yameanza kutoa matokeo chanya ambapo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimeanza kupokea uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema TIC imesajili miradi mipya ya uwekezaji 256 kwa mwaka 2021 ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 3.749 ambayo inatarajiwa kutengeneza ajira 53,025.
Wakati huo huo, Tanzania na Ufaransa zimetia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Kampuni ya Ujenzi ya Bouygues Batiment International, ya kufanya upembezi yakinifu wa ukarabati wa Terminal II ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo ya Viwanja vya Ndege wa Ufaransa, Eric Fleurisson na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania Dk. Ally Possi.
Ufaransa ni moja ya nchi zilizofanya uwekezaji mkubwa nchini ikiwa imewekeza katika miradi takriban 40 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3.4 na hadi sasa imezalisha ajira 1,885.
Na MWANDISHI WETU