RAIS Samia Suluhu Hassan, ameagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Happi, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mkoa huo, kujitathimini sababu ya kukwama kukamilika miradi ya maendeleo, licha ya serikali kutoa fedha.
Pia, ametangaza kiama kwa wakuu wa idara za halmashauri katika mkoa huo.
Aidha, Rais Samia ameagiza kupatiwa ripoti ya utendaji kazi za wakurugenzi wote nchini, waliokuwa katika kipindi cha uangalizi wa miezi sita ili hatua zichukuliwe kwa wale walioonekana kulegalega.
Akizungumza na wananchi wa Musoma Mjini wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia alimtaka mkuu wa mkoa huo, kutoogopa kuwashughulikia wale ambao wanakwamisha miradi ya maendeleo.
“Nilichokisikia hapa kwa kiasi kikubwa kuanzia kwa Mkuu wa Mkoa ni kama ubadhirifu umeota nilikuwa nikufyatue hapa, lakini mwenyewe umeanza kwa kuyasema na hii inanionyesha kwamba unayafuatilia, lakini vinginevyo kwa taarifa nilizokuwa nazo nilikuwa nikufyatue.”
“Kuna fedha nyingi zinaingizwa katika mkoa huu, lakini kuna ufujaji, kuna ucheleweshaji utekelezaji wa miradi inayoletwa kwa fedha hizo na hili linafanywa na wanaMara mpo, viongozi wa mkoa wapo, wakuu wa wilaya wapo, halmashauri zipo lakini bado mambo yanaendelea,” alisisitiza.
Alieleza kuwa wakurugenzi wa halmashauri waliokuwa katika matazamio ya miezi sita tangu walipoteuliwa mpaka itakapofika Februali 18 mwaka huu, apelekewe taarifa ya utendajikazi wao.
“Nimemwambia Waziri wa TAMISEMI aniletee taarifa ya kazi walizozifanya wakurugenzi katika maeneo mbalimbali, taarifa ile itatuambia mkurugenzi gani ndiye nani siye na hapo ndipo tutaamua nani abaki nani aondoke pamoja na wale niliowaondoa juzi,’ alisisitiza.
Rais Samia alisema serikali inafuatilia kwa karibu fedha zinazotolewa halmashauri kwa utekelezaji miradi ya maendeleo, ambapo aliagiza kuvunjwa mkataba kwa mkandarasi wa mradi wa barabara ya Makutano Juu-Samzate inayojengwa kwa kilometa 50, kwani mkandarasi amekuwa akisuasua.
“Serikali inatoa fedha nyingi kuondosha shida kwa wananchi na haki yao kuhudumiwa na ndugu zao wana Mara, sasa ndugu zao mnapojali ubinafsi na kuacha kushughulikia kero za wana Mara, mkoa wenu hautakwenda mbele mtabakia na miradi ile ile ya miaka mingi haishughulikiwi. Tatizo sio serikali, tatizo ni wana Mara wenyewe.
Aliongeza: “Mngechangamka kwa kusema na kusimamia matatizo haya yangejulikana mapema serikalini na hatua zingechukuliwa, lakini mnakaa na kuangalia mambo yanavyoharibika. Mnakunja mikono na kulalamika, mnategemea nani kule makao makuu atajua yale yanayoendelea huku, ni nyinyi wana Mara katika ngazi zenu tofauti. Kuna wabunge, kuna meya, wakuu wa wilaya, mkuu wa mkoa.”
Alisema lakini viongozi wanasuburi ziara ya rais au waziri ndipo waseme na kuwarudisha nyuma wananchi wa Mkoa wa Mara, ambapo alisisitiza ikifika 2023 bado mkoa huo ukibaki kwenye hali hiyo atakwenda kuwaambia wananchi wasiwachague viongozi waliopo.
“Nakuja kuwachongea kwa wananchi wasiwateue kwa sababu mnateuliwa kwa binafsi zenu na sio kwa maendeleo yao. Jirekebisheni shughulikieni shida za wananchi, fedha nyingi tunaleta zinaibiwa, zinaliwa huku mkiangalia hakuna uchunguzi hakuna kinachoendelea mpaka viongozi waseme hapa fanyeni uchunguzi hapa wasimamishe, hatuendi hivyo,” alionya.
Alieleza kuwa: “Miradi inayoletwa kwenu ni ya kwenu na sisi tunapiga kelele huko kwetu kama miradi haiendi, simamieni miradi huduma kwa wananchi zipatikane ni aibu fedha nyingi za maji zimeletwa zimeliwa lakini mmekaa tu. Wana Mara hamuwatendei haki wananchi wenu hata kidogo, badilikieni simamieni miradi kama kujinufaisha imetosha.”
VIGOGO KITANZINI
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwachunguza watumishi kutoka wizara hiyo na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) waliohusika kuongeza takwimu za uongo za makadirio ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere.
Alisema watumishi hao waliandika ripoti kwamba zinahitajika sh. bilioni 27 kuendelea na ujenzi, wakati uhalisia fedha zinazohitajika ni sh. bilioni 24.
“Tunakuomba Rais hizo sh. bilioni 24 usitupatie kwanza mpaka tutakapojiridhisha kiasi kamili cha fedha kinachohitajika. Tunaomba pia Waziri wa Maji atusaidie kwa sababu eneo la maji nako wameandika gharama kubwa, lakini pia kwenye umeme wameongeza gharama kutoka sh. bilioni tano hadi 10,” alieleza.
Kuhusu maendeleo ya sekta ya afya, alisema katika kipindi cha miezi tisa ya Rais Samia amejenga vituo vya afya 233 wakati miaka mitano iliyopita serikali imejenga vituo vya afya 487.
Alifafanua kuwa Rais Samia ametoa sh. bilioni 44 za ujenzi wa hospitali za mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe, Songwe, Katavi na Mkoa wa Mara.
Aliongeza kuwa sh. bilioni 31.7 zimetolewa kujenga hospitali za kanda mikoa ya Mbeya, Mtwara na Chato huku sh. bilioni 333.8 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
Hata hivyo, alisema pamoja na serikali kutoa fedha hizo, bado hali ya upatikanaji dawa bado hairidhishi, hivyo amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kufuatilia upatikanaji dawa.
Ummy alisema mpango wa serikali ni kuzifanya Hospitali ya Kanda Chato, kuwa bobezi kwa magonjwa ya moyo, Hospitali ya Julius Nyerere ijikite katika matibabu ya mifupa.
Kuhusu hali ya ugonjwa wa Uviko-19, alisema takwimu za kuanzia Januari 29 hadi Februali nne mwaka huu, walipimwa wagonjwa 6,838, ambapo watu 206 walibainika kuambukizwa virusi vya Uvuko-19.
“Katika wagonjwa hao, 71 wamelazwa, 69 wamebainika kuwa hawajachanjwa na wanne pekee ndio waliochanjwa. Kati ya wagonjwa watatu waliofariki dunia katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Manyara wote walikuwa hawajachanja,” alieleza.
Waziri Ummy alitoa rai kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 ili kuendelea kujikinga dhidi ya maradhi hayo.
MKUU WA MKOA
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara, Happi alimuomba Rais Samia kusaidia kufumua wakuu wa idara katika Halmashauri za Wilaya za Musoma Vijijini, Tarime na Bunda kwa sababu wamekuwa wakijihusisha katika vitendo vya ubadhirifu vinavyochangia ucheleweshaji miradi ya maendeleo.
Akitolea mfano Halmashauri ya Tarime ambako fedha za maendeleo zinazotolewa kupitia mgodi wa dhahabu wa Nyamongo zimekuwa zikifujwa.
Kwa upande wa Bunda Vijijini alisema zaidi ya sh. milioni 400 zimelipwa kwa mzabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ambavyo bado havijaletwa huku watendaji wa halmashauri hiyo wakidai kwamba hawana eneo la kutunza vifaa hiyo.
“Tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwamba umetuleta wakurugenzi na wakuu wa wilaya wapya, lakini hawa wakuu wa idara ni wafujaji, wanapaswa kuondolewa kwani wengi wao wamekaa muda mrefu. Nilikuwa nazungumza na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, kule kuna bwana fedha ambaye anakusanya fedha kisha baadhi kuzitumia kabla hazijapelekwa benki,” alieleza huku akishangiliwa na wananchi katika mkutano huo.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Happi alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa 708, huku sh. bilioni 4.8 zimetolewa kununua gari ya wagonjwa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyarere, vifaa vya EMD, sh. milioni 770 za ununuzi wa vifaa vya ICU na sh. milioni 133 za kununua vifaa vya mifumo ya ICT.
Aidha, alisema serikali imetoa sh. bilioni tatu kwa ajili ya uendelezaji wa hospitali za wilaya huku vituo vya afya 10 vimejengwa kupitia fedha za tozo ambapo kila kituo kimepewa sh. milioni 250.
KATIBU MKUU AFYA
Akizungumzia ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi, alisema Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ilianza kujengwa mwaka 1975 kwa usanifu kisha ujenzi ulianza mwaka 1980.
Alibainisha kwamba awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa msingi na sakafu, awamu ya pili iliyoanza mwaka 2011 hadi 2018 ilihusisha ujenzi wa kuta, nguzo, sakafu, lifti na ngazi huku awamu ya tatu iliyoanza mwaka 2018/2019 ilihusisha ujenzi wa kitalu C.
Alieleza kuwa awamu ya nne iliyoanza mwaka 2019 na inatarajiwa kukamilika Februari, mwaka huu, ilihusisha upanuzi wa majengo, usimikaji wa mfumo wa gesi tiba na ujenzi wa majengo ya huduma saidizi kama jengo la kuhifadhi maiti, chumba cha jenereta na kichomea taka.
Profesa Makubi alisema hadi sasa ujenzi wa hospitali hiyo umefikia asilimia 58, huku awamu ya tano ya ujenzi ikitarajiwa kutumia sh. bilioni 24 kwa ajili kukamilisha ujenzi wa majengo A na B, kukamilisha mfumo wa umeme, uzio, barabara na maegesho ya magari.
Hata hivyo, alisema mpango wa serikali ni kuifanya hospitali hiyo kuwa bobezi kwenye tiba ya upasuaji mifupa na ajali.
MBUNGE MUSOMA MJINI
Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedastus Manyinyi, alisema huwezi kuzungumzia maendeleo kuanzia mwaka 2015 bila kumtaja Rais Samia.
Alisema maeneo mengi ya barabara za Musoma Mjini yamejengwa kwa barabara za lami na sasa wamepatiwa sh. milioni 380, ambazo zimewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi.
Katika sekta ya afya, alieleza kuwa zimetolewa fedha za ujenzi wa vituo vya afya, huku sh. bilioni tatu zikitolewa kuboresha huduma Hospitali ya Mwalimu Nyerere.
“Musoma Mjini mtu akiugua, kituo cha afya kipo, zahanati zipo, hospitali ya wilaya, mkoa na akizidiwa kuna hospitali kubwa ya rufaa,” alisema Manyinyi.
Alisema itakapofika Juni mwaka huu baada ya kukamilika mradi wa usambazaji maji, hakutakuwa na eneo lolote la mji huo ambalo halitakuwa na huduma ya maji safi na salama.
NA MUSSA YUSUPH, MUSOMA