RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuondoka nchini kesho Novemba 10, 2021, kwenda Cairo nchini Misri, kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, imesema ziara hiyo inatokana na mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah Al Sisi, ambapo akiwa nchini humo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake huyo.
Imesema kuwa, mazungumzo hayo kati ya Rais Samia na Rais Sisi yatahusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Misri ikiwemo nyanja za diplomasia, uchumi, siasa, elimu, utalii na huduma za jamii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia na Rais Sisi, pia wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa mkataba mmoja na hati saba za makubaliano kati ya nchi hizo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Profesa Wineaster Saria Anderson, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Profesa Anderson anachukua nafasi ya Profesa Eleuther Mwageni ambaye alifariki dunia Julai mwaka huu. Uteuzi huo umeanza Novemba 7, mwaka huu.
Na MWANDISHI WETU