RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itajenga kiwanda cha kuzalisha chanjo, ukiwa ni mpango wa muda mrefu wa kukabiliana na ugonjwa wa Virusi vya Corona (Uviko-19) na magonjwa mengine.
Rais Samia aliyasema hayo mjini Brussel Ubelgiji, wakati akizungumza na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Charles Michael.
Alisema dhamira yake ni kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji na msambazaji mkuu wa chanjo, katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi washirika.
Rais Samia ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa mwaliko maalumu wa Rais huyo wa Baraza la EU, alisema kufikia mwaka 2030 serikali itatumia sh. bilioni 216 kuingiza chanjo, hali inayoonyesha umuhimu wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya chanjo.
Hata hivyo, aliliomba baraza hilo kuendelea kuisaidia Burundi, akisema EU ina wajibu mkubwa wa kuimarisha utulivu na maendeleo kwa mataifa jirani.
“Utulivu wa Burundi, ni mzuri kwa nchi za maziwa makuu, Ulaya na Dunia kwa ujumla,” alisema Rais Samia akiwa nchini Ubelgiji.
Tangu kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na baraza la EU mwaka 1975, serikali imepokea misaada ya maendeleo yenye thamani ya sh. trilioni 5.98, hivyo baraza hilo litabaki kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania.
Na MWANDISHI WETU