MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuviboresha na kuvipa hadhi vyombo vya habari vya Uhuru Media Group (UMG), ili viwe na ushindani katika soko.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, wakati akitoa salamu za Rais Samia, alipozungumza na wafanyakazi baada ya ziara ya kuvitembelea vyombo hivyo.
“Rais Samia, ana nia njema, thabiti na anajipanga kuviboresha vyombo hivi, ili vifanye kazi kisasa na katika mazingira bora,” amesema Shaka.
Ameongeza kuwa, kiongozi huyo anavishukuru na kuthamini mchango wa vyombo hivyo na watumishi wake kwa jamii na CCM kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Shaka, ziara yake hiyo ni mwanzo wa ziara zake katika vyombo vyote vya habari nchini, na kuwa ameanza na vyombo vya Uhuru Media na Africa Media Group kampuni inayomiliki Channel ten na Redio Magic, kujifunza utendaji kazi.
“Nilipopanga kufanya ziara katika vyombo vya habari, nimeona nianze na hivi vya nyumbani ili nijifunze utendaji kazi, ndiyo niende nje,” amesema Shaka.
Amesema CCM kwa ujumla inatambua na kuthamini kazi iliyofanywa, inayofanywa na itakayoendelea kufanywa na watumishi wa vyombo hivyo.
Hivyo, ametaka mshikamano miongoni mwa watumishi wa taasisi hizo, akisema ndiyo msingi wa maendeleo.
“Tuwe wamoja tutangulize dhamira njema, tunawategemea kila mmoja kwa nafasi yake na naamini mnaweza, lakini nataka kuwaambia jahazi la UHURU lazima liende kwa umoja na mshikamano,” Shaka.
Hata hivyo, Shaka ameahidi kushirikiana na watumishi hao wakati wote, na kuwa hatachoka kufanya ziara na kusikiliza kero na kutatua changamoto.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group (UMG), Ernest Sungura, amesema bidhaa za magazeti ya kampuni hiyo, zinazalishwa na habari zenye shabaha ya kuunga mkono dhana ya Kazi Inaendelea na Uchumi wa Bluu.
katika ziara hiyo, Shaka alitembelea Africa Media Group kampuni inayomiliki Channel ten na Redio Magic, pia Ofisi za Redio Uhuru na Magazeti ya Uhuru.
PICHA: Katibu wa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya UMGL. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Siasa katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa UMGL, Angel Akilimali na Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa UMGL , Ernest Sungura.