RAIS Samia Suluhu Hassan, ameungana na viongozi mbalimbali duniani kumtakia kheri aliyekuwa Waziri Mkuu Dk. Salim Ahmed Salim kwa kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa, huku akimtaja kama mtumishi mahiri wa umma wa Watanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mtandao wa twitter, viongozi hao walimtaja Dk. Salim kuwa kiongozi mahiri kwa Afrika na Dunia, aliyejitoa mstari wa mbele katika kutafuta amani, uhuru katika maeneo mbalimbali ya nchi duniani ikiwemo China, Ethiopia na Eritrea. Dk. Salim alizaliwa Januari 23, 1942.
Rais Samia aliweka andiko katika mtandao wake wa Twitter, ”Kheri ya siku ya kuzaliwa kwa Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim, mtumishi mahiri wa umma wa Watanzania, Afrika na Dunia kwa zaidi ya miongo minne. Katika siku hii adhimu ya kumbukumbu ya miaka 80 ya kuzaliwa kwako, tunakushukuru kwa utumishi uliotukuka kwa nchi yetu.”
Mbali na Rais Samia, viongozi wengine walioweka maandiko yao ya kumtakia kheri Dk. Salim ni pamoja na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye aliweka andiko katika mtandao wake wa Twitter kwa kuambatanisha picha akivishwa nishani na Dk. Salim.
Katika andiko hilo, Rais Ramaphosa aliandika ”Kheri Dk. Salim Ahmed Salim, Katibu Mkuu wa zamani wa OAU na Waziri Mkuu wa Tanzania, kwa kutimiza miaka 80.
Umekuwa bingwa mpambanaji wa umoja wa Afrika na Uhuru na rafiki wa kweli wa Wananchi wa Afrika Kusini.”
Pia, Mshauri wa Rais wa Marekani, Joe Biden, Balozi Susan Rice ambaye ni Mshauri wa Sera za Ndani za Rais Biden, aliandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa ”Kwako Dk. Salim. Kheri ya miaka 80 ya kuzaliwa. Nitaendelea kukukumbuka kwa juhudi zako zisizochoka za kumaliza vita baina ya Ethiopia na Eritrea.
Naye, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, aliandika katika mtandao wake wa Twitter juu ya Dk. Salim ” Balozi, Waziri, Waziri Mkuu na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu wa muda mrefu wa OAU. Salim Ahmed Salim umetimiza miaka 80. Nakutakia maisha marefu ili niendelee kuona juhudi ya maendeleo yako.”
Wengine waliotoa salamu hizo ni pamoja na mwanasiasa mkongwe nchini, Profesa Mark Mwandosya, aliyemtakia kheri Dk. Salim kwa kutimiza miaka 80, huku akimtaja alama ya maendeleo ya uongozi kwa Tanzania kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwa nchi kitaifa na kimataifa.
Balozi Peter Kallaghe, naye aliungana na wanasiasa wengine kumtakia na kusheherekea miaka 80 ya Dk. Salim kuwa anashukuru kwa yeye alikuwa msaidizi wake wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na kwamba ni kiongozi bora na mfano kwa watu wengi, Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda.
Kwa upande wake, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, aliandika katika mtandao wake wa Twitter ”Nakutakia kheri Dk. Salim Ahmed Salim katika kumbukumbu yako ya kuzaliwa. Mwenyezi Mungu akupe afya njema na maisha marefu. Watanzania tunajivunia utumishi wako uliotukuka ndani na nje ya nchi na tunakushukuru kwa kutujengea heshima Duniani”.
Na Hamis Shimye