UZALISHAJI wa zao la Pamba katika Mkoa wa Katavi bado uko chini hali iliyopelekea mwekezaji wa kiwanda cha pamba kubadili matumizi ya fedha za kununulia zao hilo kwa kuzielekeza kwenye kununua zao la mahidi.
Kwa takwimu za uzalishaji wa zao hilo Mkoa wa Katavi kwa msimu wa kilimo 2020/21 ni kg 2,173,399 zimezalishwa na kufanya kiasi hicho kuwa ni kidogo ukizingatia soko la zao hilo liko wazi kupitia mwekezaji wa NGS Investment Co Ltd kilichopo Wilaya ya Tanganyika kikiwa na uhitaji wa kg Mil 50 wa zao hilo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Rodrick Mpogolo, kwa niamba ya Mkuu wa Mkoa Mwanamvua Mrindoko, amesema hayo katika Manispaa ya Mpanda Mkoani wakati wa kufungua kikao cha wadau wa kilimo cha pamba kilicholenga kutoa hamasa na elimu ya kuzingatia uzalishaji wenye tija uliotolewa na bodi ya pamba Tanzania.
Mpogolo amesema, msimu wa maadalizi wa kilimo cha pamba umeanza na zoezi la uhamasishaji wa kutoa elimu kwa mkulima ni muhimu kwa Mkoa kutokana na uzalishaji wa zao hilo kuwa chini kwa kuzingatia takwimu za kg zaidi ya mil 2 ikiwa ni hasi ya kama Kg mil 47 hadi Kg Mil 48. Ikiwa sawa na kupewa fedha zako na kushindwa kuzichukua.
“Nitoe tu kwa wasitani kama kg 1 ya pamba inauzwa kwa Tsh 1,000/- ukizidisha mara Kg mil 50 ni sawa sawa na bilioni 50 ambazo zinaingia kwenye mkoa wetu, sisi hatujawaada wakulima kuchukua hizo billion 50”. alisema Mpogolo

Amefafanua kuwa, mkoa huo bado unatatizo na kinachotakiwa kufanywa na watalamu, bodi ya pamba Tanzania na mwekezaji kuwaunganisha wakulima waingie kwenye kilimo cha pamba cha Kisayansi ili wazichukue hizo fedha ziingie katika mifuko yao na kuboresha kipato cha familia na mkoa wa Katavi.
Ameongeza kuwa “Nilipata kutembelea kile kiwanda cha NGS, Meneja akaniambia kuwa anazo pesa benki kwa ajili ya kupeleka kwa wakulima lakini kwa kuwa hakuna pamba sasa amelazimika kuanza kuchukua mahindi”
Licha ya kuushukuru ujio wa bodi ya pamba Tanzania kupitia balozi wake Aggrey Mwanri na watalaamu wengine amesema kwenye utekelezaji wa malengo ya kilimo wamefanikiwa kugawa mbegu za pamba kwa msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2021/22 na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta hiyo kuingia shambani na kuacha kukaa ofisini na kupunguza kuandika na kwenda kufanya kazi kwa wakulima.
Renatus Luneja, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, amesema kampeni hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25, ambayo inawataka kuzalisha tani milioni moja za pamba ifikapo mwaka 2025, ili kufikia malengo hayo wameweka mikakati ya kuhamasisha wakulima kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao la pamba.

Ameeleza kuwa sehemu nyingi wakulima huzalisha wastani wa kg 300 za pamba kwa hekali moja ikiwa afadhari kwa mkoa wa Katavi huzalisha wastani wa kg 500 za pamba kwa hekali moja.
Hivyo uwezo wa mbegu kwa mujibu wa tafiti angalau wasitani wa kg 1,000 zinatakiwa kuzalishwa kwa hekali moja na kusaidia kufikia malengo ya tani milioni moja kitaifa.
Kwa upande wake Balozi wa zao la pamba Tanzania, Aggrey Mwanri, amesema pamba ni zao muhimu la biashara ambalo linaliingizia taifa fedha za kigeni na wameendelea kufanya kampeni katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara na Tabora ambapo wamekuwa wakiwahimiza wakulima kufanya kilimo cha kisayansi.
Na George Mwigulu, Katavi