MKUU Wa Mkoa Dar es Salaam, Amos Makalla, ameonyeshwa kuduwazwa na kusuasua kwa mchakato wa umaliziaji wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti.
Makalla aliyasema hayo alipotembelea machinjio hayo.
Hiyo ni mara ya pili kwa mkuu wa mkoa huyo kufanya ziara katika eneo hilo.
“Mradi huu ulikuwa katika bajeti ya awamu ya tano na kuendelea awamu ya sita kwa matarajio ya kuchinja ng’ombe 1000, mbuzi 1000 na kondoo 500 kwa siku, kwa ajili ya soko la ndani na kusafirisha nchi zingine hasa, Oman na Dubai.
“Mchanjio hayo hayajaanza kufanya kazi kwa sababu ya kukosa chumba cha baridi (cold room) cha kuhifadhi nyama hizo, hivyo haiwezi kutumika,” amesema.
Amemshauri Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, kuusimamia mradi huo hadi utakapoanza kufanya kazi.
Amesema alitarajia machinjio hayo angeyakuta yameanza kufanya kazi ya kuchinja ng’ombe, kondoo na mbuzi ila kilichokamilishwa ni majengo.
“Nilikuwa nafuatilia ahadi kwa Waziri Mkuu iliyotolewa na watendaji wa machinjio, alitarajia kufika Julai Mosi, ungekuwa umekamilika na mimi nilipokuja, mliniahidi Julai 27, mwaka huu utakuwa umekamilika kwa sasa naona hali ni ile ile,” amesema.
Makalla amemwambia Kaimu Mkurungezi wa Jiji la Ilala, Tabu Shaibu na timu ya manunuzi kukaa kikao na kutafuta mkandarasi atakayekamilisha ununuzi wa vifaa vinavyohitajika ili chumba cha baridi kikamilike, kianze kufanya kazi kama yalivyo matarajio ya wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji alitoa ahadi kwa mkuu wa mkoa kwamba, ifikapo Septemba 13, mwaka huu, watakuwa wamepata mkandarasi ili aendelea na mikakati mingine ya ununuzi wa vifaa hivyo nje ya nchi na kukamilisha chumba cha baridi.
Na CHRISTOPHER LISSA