MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ameielekeza ofisi ya madini mkoani humo kufuta leseni za uchimbaji ambazo hazifanyiwi kazi ili wapewe wengine ambao wanaweza kuzitumia.
Aidha, amesema ni utaratibu wa kisheria hivyo ni utekelezaji wa sheria huku akiwataka wadau wanaotaka kuwekeza kwenye madini kujitokeza katika fursa hiyo.
Ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Simiyu (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bariadi conference mjini hapo huku akiongeza kuwa kazi ya maeneo ya machimbo imezidi kuongezeka na tayari baadhi ya halmashauri zimeanza zoezi la uchimbaji baada ya kupata leseni.
“Halmashauri zetu tumezishawishi na zimefanya baadhi ikiwemo ya Bariadi sasa hivi ni moja ya halmashauri ambayo inapata fedha kama wachimbaji wa madini ni seme tu kwamba halmashauri zingine zote mkoani hapa ( Simiyu) zitanye pakubwa kwasababu hii ni fursa lakini vilevile wadau wa maendeleo wote mnaalikwa ” amesema Kafulila na kuongeza kuwa :
“Ujumbe ni kwamba kuna fursa kubwa katika eneo hilo hii milipuko ya madini inajitokeza karibuni kila mwezi unasikia kuna mahala tayari madini yamelipuka kwa hiyo tafsiri yake hii ni fursa “amesema Katulila
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Halid Mbwana, amesema wamepokea leseni mbili moja ikiwa Gasuma na nyingine katika kijiji cha halawa na tangu Desemba 1 ,2021, wameanza uzalishaji kwenye eneo la halawa na mpaka sasa shughuli zinazofanyika ni pamoja na uchimbaji mdogo kitu ambacho kwa wale wachimbaji waliowekwa na halmashauri hiyo wanachukua maeneo na kuanzisha maduara ya kuchimba dhahabu na mpaka Desemba 27, 2021 walikuwa na maduara 92 ambayo yamesajiliwa na yana jumla ya watu 187 ambao wanahusika kuchimba maduara na hizo ni ajira za moja kwa moja ambazo zimezalishwa kupitia leseni ya halmashauri hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Adrian Jungu, amesema tayari wao wana leseni ya uchimbaji eneo la Gasuma na wana zaidi ya hekari 30 huku mategemeo yao baada ya kuanza uzalishaji watazaliza ajira zaidi ya 100 kwa vijana na wanawake zaidi ya 50 kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula ambapo ameongeza kuwa eneo hilo ni la kimkakati kwa maana ya kuongeza ajira na mapato ya halmashauri huku shabaha yao ikiwa kuipeleka halmashauri hiyo mbele zaidi kwa kutengeneza vyanzo vipya vya mapato.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliopata ajira kupitia halmashauri ya wilaya ya Bariadi wamesema wamepata fursa ya kuona neema ya madini yanayozidi kuibuka kila mara mkoani humo.
Na Anita Balingilaki ,Simiyu