MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla, amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Kata na Mitaa kuhakikisha maeneo yote waliyoondoka Machinga yanafanyiwa Usafi na kuweka uangalizi wa kutosha ili yasivamiwe upya.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao na Watendaji kata na Mitaa kuhusu tathimini ya zoezi la kuwapanga Machinga ambapo amesema zoezi hilo linakwenda vizuri kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Aidha, RC Makalla amezitaka Halmashauri za Dar es salaam kuzitumia kampuni zilizopewa kazi ya Usafi kwenye maeneo husika kutekeleza zoezi hilo la usafi ndani ya wiki moja.
Kuhusu Wafanyabiashara waliokubali kuvunja Vibanda na sasa wanapanga bidhaa zao Chini kwenye maeneo yaleyale yaliyokatazwa RC Makalla amepiga marufuku utaratibu huo na kuwataka kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa.
Pamoja na hayo RC Makalla amezielekeza Taasisi zote za Umma ikiwemo Shule, Vyuo, Mashirika, Hospital na nyinginezo kuhakikisha hawaruhusu Wafanyabiashara kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa huku akiwaelekeza TANROAD na TARURA kuzilinda Barabara zao zisivamiwe upya.
Sanjari na hayo RC Makalla amesema ifikapo October 30 asionekane Mfanyabiashara yoyote akiendesha biashara katika maeneo yaliyokatazwa hivyo amewataka kutumia muda wa nyongeza uliotolewa kuhama.