MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amewaagiza wananchi wa mkoa huo kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi mapya ya corona ambayo yameanza kwa kasi katika nchi jirani.
Makalla alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari katika Manispaa ya Ubungo ambapo aliwataka wananchi kuvaa barakoa wakati wote wanapokuwa katika mabasi, daladala, sokoni na maeneo yaliyo na mikusanyiko ya watu wengi.
Alisema hivi karibuni kupitia kwa mkurugenzi wa Kinga, serikali ilitoa taarifa ya kuwepo kwa mlipuko wa wimbi la tatu la ugonjwa wa corona katika nchi za Afrika ambapo taarifa imetaja kuwepo kwa viashiria vya wimbi la tatu nchini.
“Kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kati ya mkoa huu na nchi jirani, napenda kuchukua nafasi hii kutoa rai kwa wananchi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari ya kujikinga na corona,” alisema.
Makalla alisema tahadhari ambazo wananchi wanapaswa kuzichukua ni kuvaa kwa usahihi barakoa kila wakati katika maeneo yenye mikusanyiko, vyombo vya usafiri, katika hafla, mikutano, vituo vya kutolea huduma za afya, maofisini, baa, migahawani na darasani.
Aliwataka wasimamizi wa taasisi mbalimbali, usafiri wa majini, nchi kavu na maeneo yote yenye msongamano wa watu kuweka miundombinu ya maji tiririka na sabuni.
“Ndugu zangu wananachi mnaombwa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya, mara upatapo dalili za uviko ambazo ni homa kali, mafua, kikohozi, uchovu mkali, kushindwa kupumua, kushindwa kunusa na kupoteza uwezo wa kuhisi ladha ya chakula,” alisema.
Mkuu huyo aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kwani huimarisha kinga ya mwili.
“Watu waliopo katika hatari zaidi ya kupata madhara makali ya covid 19, tunapaswa tuwalinde kabisa hasa wazee, wenye magojwa sugu kama vile shinikizo la juu la damu, kisukari, kifua kikuu na magojwa ya moyo,” alisema.
Pia, Makalla aliwataka wakuu wa wilaya, wakuu wa taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia maelekezo hayo kikamilifu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Mfaume, aliwataka wananchi kufuata maagizo wanayopewa na wataalamu wa afya ili kujikinga na maambikizi ya covid 19.
Dk. Mfaume alisema serikali katika kujiandaa na mapambano ya ugonjwa huo imeendelea kuboresha mahitaji muhimu katika hospitali zake kama vile kuongeza mashine za kupumulia na mahitaji mengine.
Dar es Salaam
Na RESTITUTA MARTIN