MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amesema ili kuwe na mafanikio ya kweli katika mapambano dhidi ya rushwa ni lazima ifanyike tathmini kujua athari zake na ili kupambana nayo ni lazima uichukie.
Aidha, Malima ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tanga na Chama cha Skauti Tanzania kwa kuanzisha ushirikiano na vijana katika mapambano dhidi ya rushwa.
Malima amesema hayo, wakati akifunga semina ya mwongozo wa mafunzo kwa wawezeshaji kufundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa.
Amesema usipotafakari kwa upana athari za rushwa ndiyo unakutana na watu wanaotafuna fedha za miradi au kuelekeza katika matumizi yasiyo sahihi.
“Nawaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Tanga, nendeni mkaufanyie kazi mwongozo huu ufike wilaya zenu maeneo yote.” Amesema RC Malima.
Kwa upande wake Mkuu wa Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza, amesema mwongozo huo unamwezesha mtoto kuanzia miaka mitano hadi chuo kikuu kutambua athari za rushwa ambapo baadhi ya vijana ambao tayari wamepata mafunzo wamesambazwa kila wilaya ili kunusa harufu za rushwa.
Amesema endapo kila mmoja atachukia rushwa na kutekeleza wajibu wake nchi itabadilika.
Amesema ni vigumu kumfundisha mtu mzima kutii sheria lakini ukianzia kwa watoto na vijana inakuwa rahisi.
“Tuliona taasisi yetu inaweza kushirikiana na wengine katika kutokomeza rushwa tukaona tuwashirikishe wenzetu wa Takukuru tuanze kufundisha vijana rushwa ni nini na athari zake.
“Tuwaeleweshe wanafunzi kujitambua na nini mchango wake kwa taifa. Rushwa imetuchelewesha mno kufikia maendeleo, tukawe mfano katika maeneo yetu na pale unapoona kiashiria cha rushwa basi toa taarifa,” amesema Mahiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Zainab Bakari, amesema skauti ana uwezo wa kutambua adui kabla hajaleta madhara na Takukuru inaweza kunusa harufu ya rushwa na kuzuia hivyo ushirikiano wa Takukuru na Skauti utaleta tija.
Na Susan Uhinga