MKUU wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, ameonya baadhi ya mabaraza ya ardhi ‘mizigo’ kuwa yatapimwa kwa kazi zao na hatasita kuyavunja yasipowajibika.
Kunenge alisema amejipanga kuyasafisha mabaraza yasiyofanya kazi zake ipasavyo, yanayopindisha sheria na kutotenda haki.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020-2025) katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, Kunenge alisema wajumbe wasiotimiza wajibu wao wanaondoa imani kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema wajumbe wa mabaraza hayo wapo kwa lengo la kutatua migogoro ambayo haiwezekani na kuonya kwamba jambo la walengwa kwenda mkoa, wakati mabaraza hayo yapo na kama wapo mizigo waondolewe.
Alionya kuna baadhi ya watu wanakwamisha maendeleo kupitia mwamvuli wa Chama, hivyo aliomba ushirikiano na CCM ili kuchukua hatua dhidi ya watu hao.
“Migogoro ya wakulima na wafugaji na ardhi inakuwa mingi kutokana na kutofuata sheria. Migogoro ya wakulima na wafugaji ni mwiba na changamoto inayomnyima usingizi viongozi,” alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani katika mkoa huo, Kunenge alisema upo vizuri kwa sekta zote na changamoto zilizopo serikali inaendelea kuchukua hatua.
Naye, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno, alisema Chama kina uhusiano mzuri na serikali ya mkoa huo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Gunini Kamba, akizungumzia masuala ya chanjo ya corona, alisema zaidi ya watu 15,000 wamechanjwa mkoani humo na hali zao za kuridhisha.
“Tumekuja kuongea na halmashauri, tushirikiane kuhamasisha wananchi wajitokeze kupata chanjo ili kupambana na ugonjwa huu kwa kuwa upo, tujihadhari, “alisisitiza Dk. Gunini.
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha