WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), umesema umeme hapa nchini ni mmoja na kwamba madai yaliyopo, kuwa umeme unaoitwa wa REA na umeme wa TANESCO ni tofauti hata kwa uwezo na ufanisi ni uzushi mkubwa.
Mhandisi wa Umeme kutoka REA, Jensen Mahavile, akizungumza na UhuruOnline katika banda la wakala huo lililopo viwanja vya maonyesho ya Sabasaba, amesema kupungua kwa ufanisi wa umeme eneo fulani hususan vijijini kunatokana na mtawanyo mkubwa, ambao hata hivyo unatatuliwa kwa kufungwa transfoma kila baada ya umbali fulani.
“Transfoma hizi ndizo huongeza nguvu ya umeme ule, ambayo huonekana kupungua kutokana na kutawanywa kwenye watumiaji wengi kwa eneo kubwa au dogo, kutegemeana na matumizi ya umeme husika.
“Hivyo siyo kweli kwamba kuna umeme wa REA na umeme wa TANESCO, umeme ni umeme tu, REA ni wakala wa kusambaza umeme huo huo uliopewa jina mtaani kuwa ni ‘umeme wa TANESCO’ ni vyema ikaeleweka vizuri,” amesema.
Kadhalika, mhandisi huyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda hilo la maonyesho la REA, ili kupata majibu ya maswali yao kuhusu usambazaji wa umeme vijijini.