NA WILLIUM PAUL, Siha
HALMASHAURI ya Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, imewafukuza kazi watumishi sita wanaodaiwa kuisababishia halmashauri kupata hati yenye shaka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2020.
Akitangaza uamuzi huo, katika kikao cha kujadili taarifa ya CAG, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Ndaki Mhuli, alisema hati hiyo yenye shaka imesababishwa na makusanyo ya maduhuli ya sh. milioni 112.5, kutopelekwa benki.
Mhuli alisema sababu nyingine zilizoifanya halmashauri hiyo kupata hati hiyo ni kufanya marekekibisho katika mfumo wa fedha (LGRCIA) yenye thamani ya sh. milioni 624, bila kupata idhini kutoka kwa Ofisa Masuhuli.
“Pia yapo matumizi yaliyofanyika bila kuwa na viambatanisho yenye thamani ya shilingi milioni 101.5, kukosekana kwa hati ya malipo ya shilingi milioni 59.2, wakati wa ukaguzi na kukosekana kwa viambatanisho vya shilingi milioni 10 katika ujenzi wa madarasa kupitia akaunti ya kijiji cha Ngarenairobi,” alisema.
Alisema watumishi hao sita waliofukuzwa kazi ni kutoka Idara ya Fedha na Ununuzi huku wengine wanne wakikatwa fedha katika mishahara, kisha kupewa adhabu ya kupunguziwa mshahara kwa asilimia 15.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, aliwataka madiwani kwa kushirikiana na watendaji wa halmashauri kuendelea kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri ili kudhibiti hoja za CAG na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Aidha, alimtaka mkurugenzi wa halmashauri kuimarisha kitengo cha ukaguzi wa ndani kwa kukiwezesha nyenzo ili kifanye kazi kwa weledi na kuibua hoja za kikaguzi mapema na kuzitolea majibu, kabla ya kufanyiwa ukaguzi na CAG.
“Nimesikia maoni yaliyokuwa yakitolewa na madiwani kuhusu hoja za CAG sasa menejimenti zingatieni yaliyoelekezwa na baraza, kwa kuwa kazi yao ni kuisimamia na kuishauri halmashauri itekeleze wajibu wake,” alisema.
Alisema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona nchi inasonga mbele kimaendeleo, hivyo ni muhimu viongozi wakasimamia mapato na matumizi kwa manufaa ya wananchi wa Siha.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Seif Shekalage, alimuomba CAG kuzishauri halmashauri chanzo cha kuibuka hoja za kikaguzi ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.