BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeitoza faini Kampuni ya mafuta ya Lake Oil, Sh. bilioni. 3.3 kwa kukiuka sheria na kanuni za mazingira.
Pia, baraza hilo limetoa siku saba kuanzia leo kwa wamiliki wa vituo vyote ambavyo vimejengwa bila kuwa na vibali vya tathimini ya athari za mazingira kufika ofisi za NEMC kwa ajili ya kutoa maelezo kwa nini wasichukuliwe hatua.
Wakati wamiliki hao wa vituo vingine wakipewa siku saba kuanzia leo kutoa maelezo kwanini wasichukuliwe hatua, Lake Oil wametishiwa kufungiwa vituo vyote 66 iwapo watashindwa kulipa faini ndani ya siku 14.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, ambapo alibainisha kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya wananchi wanaoishi karibu na vituo hivyo kuilalamikia kampuni ya Lake Oil kujenga vituo vyao karibu na makazi ya watu.
Alisema kujenga vituo vingi vya mafuta maeneo mbalimbali nchini bila kuwa na vyeti vya tathimini ya athari za mazingira ni makosa kisheria.
“Tunaendelea kufanya uchunguzi nchi nzima na wote tutakao wabaini kujenga vituo bila tathimini ya mazingira watatozwa faini kama hii kwa mujibu wa sheria, kwa sababu tumegundua kwamba vituo hivi vinaota kama uyoga na hatuwezi kuendelea kubembelezana wakati elimu tumeshatoa sana,” alisema.
Alisema NEMC imebaini ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya mafuta ambavyo katika uchunguzi wao waligundua kuwa vituo vingi havina vibali vya ujenzi wala vyeti vya tathimini.
Dk. Gwamaka alitoa muda wa siku saba kuanzia leo kwa wamiliki wa vituo vyote ambavyo vimejengwa bila kuwa na vibali vya tathimini ya athari za mazingira kufi ka kwenye ofi si za NEMC kwa ajili ya kutoa maelezo kwa nini wasichukuliwe hatua.
Alisema imepita miaka 17 tangu sheria ianze kufanya kazi na NEMC ilitoa elimu kupitia njia mbalimbali lakini wenye vituo wameonyesha ukaidi, hivyo muda wa kuchukua hatua kali umefi ka.
“Kuna vituo vya mafuta zaidi ya 3,000 nchini na katika vituo hivyo havizidi 600 ambavyo vimesajiliwa na NEMC na kupata hati za tathimini, sasa kwa nchi nzima unapoongeza vituo vya mafuta bila kufuata sheria ni hatari sana,”alisema.
Kwa mujibu wa Dk.Gwamaka, kanuni zinataka umbali wa kituo kimoja cha mafuta hadi kingine usipungue mita 200 ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kutokea wakati wa dharura ya moto lakini kutokana na dharau ya wenye vituo hawazingatii kanuni hiyo.
Alisema wenye vituo vya mafuta wengi wamekuwa wakijenga na kisha kwenda kutafuta vibali baada ya ujenzi na wamekuwa wakivitafuta kwa njia za rushwa na magendo.
Dk. Gwamaka alisema wananchi wanaozunguka eneo kinapojengwa kituo cha mafuta wana haki ya kushirikishwa na kupewa elimu kuhusu namna wanavyoweza kujiokoa inapotokea dharura.
“Sheria inawataka wenye miradi kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kabla ya ujenzi wa vituo ili watoe maoni na mawazo yao.
Hiyo ni haki yao ya kisheria ambayo hawapewi na hawa watu lakini wanapata madhara makubwa ya kiafya,” alisema.
Alisema lengo ni kutaka wenye miradi hiyo kuwashirikisha wananchi na kupata kibali cha tathimini kabla ya ujenzi na kujua usalama wa kiafya wa wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo
Na REHEMA MAIGALA