RAIS Samia Suluhu Hassan amesema dunia ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha miradi ya maendeleo.
Amesema katika kipindi cha miezi sita, idadi kubwa ya wawekezaji wamejitokeza kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali, ambapo mmojawapo ni ujenzi wa kiwanda cha mbolea ambacho kinaendelea kujengwa Dodoma.
Rais Samia aliyasema hayo jijini Dodoma alipowasili akitokea Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu aliporejea nchini kutokea New York, Marekani alikohutubia Mkutano Mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa (UN), Septemba 23, mwaka huu.
“Kwa ujumla mambo yetu si mabaya, ni mazuri. Ulimwengu upo tayari kufanya kazi nasi, yale yaliyosemwa hapa ya umeme, maji maradasa na mambo mengine, nataka niwahakikishie wana Dodoma hiyo kero tunakwenda kumaliza.
“Najua kwamba ndani ya mkoa huu wa Dodoma kuna kata ambazo bado hazina vituo vya afya, niwaambie kama tutakapojipanga, vituo vya afya vitakuja, pengine hatutoweza kila kata, lakini vingi vitajengwa ndani ya Dodoma,” alisema Rais alipokuwa akizungumza na wananchi aliposimama njiani kusalimia wananchi wakati akienda Ikulu ya Chamwino.
Rais Samia alisema serikali imefanya kazi kubwa kupunguza kero ya maji kutoka saa nne au sita za upatikanaji wa huduma hiyo hapo awali, hadi kufikia saa 10 hivi sasa mkoani Dodoma.
“Nawaahidi kwamba tunakwenda kulijenga bwawa la Pargwa…na Dodoma itakuwa haina tatizo la maji. Tupeni muda, tunzeni amani na utulivu sisi tutafute fedha ili tujenge maendeleo yetu,” alisema.
Alisema kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika mkoa huo inaendelea kutekelezwa kwa kasi, ambapo mbali na barabara za mzunguko, pia serikali imepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani.
Rais Samia alisema tayari maeneo ambayo lami haijaingia, hususan mkoa wa Dodoma kazi hiyo itafanyika, kwa kuwa ni mji wa serikali.
“Kwa ujumla
serikali yenu ipo vizuri, tunakwenda kukamilisha miradi yote ya maendeleo kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi (ya CCM), lakini kuna mengine ambayo hatukujua kama wawekezaji wangekuja, wanakuja na tutaitekeleza pia. Kwa hiyo yale ya wawekezaji hayakuwa ndani ya Ilani, Ilani ilitutuma tutafute wawekezaji waje kuwekeza, nami nataka kuwaambia wawekezaji tumepata wengi mno,” alisema.
Rais Samia alisema katika kipindi cha miezi sita kumekuwa na idadi kubwa ya wawekezaji waliojitokeza kuwekeza nchini, wameendelea kuingia na wengi zaidi wataendelea kuja.
Aliwashukuru wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea.
“Sasa ndugu zangu niwashukuru sana sana sana kwa mapokezi haya, nimekuwa nikitua Dodoma kutoka safari zangu za kikazi, lakini napokewa na wakubwa tu hawa, leo nikaambiwa wananchi wanakusubiri pale nje, nikajiuliza kunani Dodoma kunani, nikaambiwa ni hotuba yako ya Umoja wa Mataifa.
“Ndugu zangu nawashukuru sana, nawashukuru sana. Naomba tuungane tushikane, tuchape kazi tujenge taifa letu, hakuna wa kutujengea bali ni sisi wenyewe. Sisi tutahangaika kule na huku, lakini Watanzania mchape kazi ili taifa letu liimarike na liende kwa harakaharaka tuweze kukuza uchumi wetu,” alisema.
Rais Samia aliwasili nchini Marekani, Septemba 18 mwaka huu, na kupokelewa kwa shangwe na furaha na baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Alishiriki mijadala mbalimbali kabla ya kulihutubia baraza hilo Septemba 23, mwaka huu na hotuba yake kupongezwa na wananchi na wachambuzi wa siasa na diplomasia wakisema imefungua milango ya Tanzania katika medani za kimataifa.
CHAMWINO
Akiwa wilayani Chamwino, Rais Samia alipokelewa na mamia ya wananchi wakiwemo viongozi wa kimila ambao walimkabidhi ngao na mkuki kama ishara ya uongozi pamoja na kamba kama ishara ya kupewa zawadi ya ng’ombe wa maziwa.

Alishukuru kwa kukaribishwa huku akiwaeleza kwamba anazifahamu changamoto za Chamwino kwa sababu naye ni Mkazi wa Chamwino.
“Nisingependa kukaa tukiwa na changamoto. Nitajitahidi changamoto tulizokuwa nazo tuweze kuzitatua, najua eneo letu hatuna soko kubwa nitahakikisha soko tunalipata. Kuna tatizo la maji tuhakikisha yanapatikana na tunaongeza vituo vya afya.
“Tulianza na kaka yetu (Hayati Dk. John Magufuli) ambaye aliipenda na kuijenga Chamwino, tuliokuja nyuma yake mwendo ni ule ule wa kuhakikisha tunakamilisha aliyoyaacha na kufanya mengine yatakayokuja,” Rais Samia aliwaeleza wananchi hao ambao walikuwa wakifurahi kumpokea kiongozi huyo wa nchi.
MUSSA YUSUPH, DODOMA na NASRA KITANA DAR