MBUNGE wa Jimbo la Makete, Festo Sanga, anatarajia kuanza ziara maalumu ya Kata hadi Kata katika Vijiji vya jimbo hilo ili kutatua, kushukuru, kusikiliza kero za wananchi na kushiriki shughuli za maendeleo.
Akizungumza na UhuruOnline, Sanga amesema baada ya kuhitimisha bunge la bajeti Juni 30, mwaka huu, ameona ni wakati wa kurejea kwa wapigakura wake.
“Baada ya kuwasilisha mawazo ya wananchi Bungeni na kuomba walivyonituma, sasa ni muda wa kurejea tena kwao kutatua, kushukuru, kusikiliza kero na kushiriki kazi za maendeleo,” amesema.
Sanga amesema ataanzia Kata ya Lupalilo, Iwawa, Bulongwa, Tandala, Luvumbu huku akibainisha kuwa ziara hiyo itakuwa ni mwendo wa kijiji kwa kijiji kuanzia Julai 8 hadi Julai 17, mwaka huu.
Mbunge huyo amesema mkutano wa kwanza unatarajiwa kufanyika Julai 8, mwaka huu, kuanzia saa Saba mchana, eneo la Tandala Mjini na Julai 12, mikutano itafanyika Ihela, Ikonda na Usagatikwa.
Kwa mujibu wa wananchi wa Makete, Mbunge Sanga amekuwa mstari wa mbele katika kutanguliza maslahi ya umma na wananchi wa jimbo hilo.