SERIKALI imesema itatekeleza ahadi zote zilizotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. Magufuli kama ilivyoahidiwa na Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan katika hotuba aliyotoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Septemba 3, 2021 na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini (CCM), Robert Maboto.
Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano ya ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Bunda kwa kuwa mpaka sasa hauna barabara za lami?.
Akijibu swali hilo, Silinde amesema Halmashauri ya Mji wa Bunda ina barabara za lami zenye urefu wa kilometa 2.22.
Barabara hizo ni Boma kilometa 1.36, Malugu kilometa 0.42, DC kilometa 0.24 na Posta kilometa 0.2. Barabara hizi zilijengwa kufuatia ahadi ya Rais wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete.
“Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Uendelezaji Miundombinu katika Miji (TACTIC) unaotarajiwa kutekelezwa katika Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji 45 ikiwemo Halmashauri ya Bunda Mji.
Programu hii itahusisha pia ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Bunda kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyoainishwa na Halmashauri ya Bunda Mji,” ameeleza Silinde.
Na SELINA MATHEW, Dodoma