SERIKALI imekisikia kilio cha wananchi wa Tarafa ya Vunta, Wilayani Same, Mkoani Kilimanjaro baada ya kutoa sh. milioni 400 za kuikarabati barabara ya kutoka Hedaru- Vunta- Mamba Miamba, yenye urefu wa kilomita 42.
Barabara hiyo awali ilitajwa kuwa ni chanzo cha wanaweke wajawazito kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha wanapokimbizwa hospitalini.
Akizungunza kwenye kikao cha kujadili fedha walizopitishiwa na bunge katika jimbo la Same Mashariki na Madiwani wa jimbo hilo, Mbunge wa jimbo hilo, Anna Kilango, amesema tayari wamekabidhia milioni 400 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo.
“Tayari serikali imeona adha wananchi wa jimbo hili wanazokutana nazo na tumetengewa milioni 500 kwa jimbo letu, pia kuna bilioni moja zimeletwa kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), ambazo zitaendelea na ukarabati kwa sasa.
“Niwaombe wananchi kuendelea kuwa wavumilivu serikali ni tulivu na sikivu itahakikisha imemaliza matatizo yote ya wananchi hasa ya barabara, afya na elimu,” amesema.
Mbunge huyo amesema ujenzi wa barabara hizo ukikamilika utasaidia kumaliza matatizo yanayowakabili wanachi hususani ya usafirishaji wa mazao kwa lengo la kujiongezea kipato pamoja na kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wakiwemo mama na mtoto.
“Serikali imeamua kuijenga barabara ya Same- Kisiwani- Mkomazi kwa kiwango cha lami ambapo sh. bilioni 4.5 zimeshasainiwa kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 5 za lami, hii itasaidia sana wananchi kusafirisha mazao yao kwa uhakika kwani TARURA nao wanajitahidi kuzifungua barabara za ndani,” amesema.
Kadhalika, ameongeza kuwa, barabara nyingine zinazotarajiwa kukarabatiwa katika kipindi hiki ndani ya jimbo hilo ni Ndungu-Lugulu na barabara ya Bwambo- Gavao- Saweni.
Na Paul William