SERIKALI inakusudia kuanza kuchukua hatua kali za kisheria, ikiwemo kifungo cha miezi sita gerezani kwa wamiliki wa makazi, viwanda na kumbi za starehe ambao maeneo yao yamekithiri kwa kelele na mitetemo.
Pia, imewaomba viongozi wa dini kupitia Kamati za Amani, kujadili namna bora ya kudhibiti kelele na mitetemo katika nyumba za ibada kwa lengo la kulinda afya za waumini wao.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, wakati akitoa taarifa kuhusu mkakati wa serikali katika kudhibiti kelele na mitetemo inayoathiri mazingira kwa jamii.
Waziri huyo amesema watakaobainika kukiuka Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, inayokataza kelele zilizopitiliza, watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miezi sita gerezani au kulipa faini ya sh. milioni moja.
Na Mussa Yusuph