WAKULIMA wa vitunguu Kata ya Mwanyahina iliyopo wilayani Meatu mkoani Simiyu, wameiomba serikali mkoani humo kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika uzalishaji wa zao hilo ili kupata tija.
Wameyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo ambapo wamesema asilimia kubwa ya wanunuzi hutumia vifungashio visivyo sahihi ambavyo vinawanyonya wakulima ,kukosa mitaji.
“Yale mashishimbi (lumbesa)wanakuja nayo yanatusababishia hasara, wao ( wanunuzi) ndio wanapata faida kupitia kwetu, na ukijaribu kuwahoji huwa wanasema bora apigwe faini lakini mzigo ufike sokoni kuliko kufungashia kwenye vifungashio vile vidogo, masoko ya uhakika na yenyewe nayo changamoto, kupanda kwa bei ya mbolea mwaka huu tumenunua mpaka laki moja ukiangalia watu hawana mitaji kwa ajili ya kuendeleza hiki kilimo cha umwagiliaji, lakini pia changamoto nyingine watu wanapambana na tembo, hawalali kama bundi” amesema Mwigulu Mboje mkulima wa vitunguu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Meatu, Albert Rutahiwa, amesema jumla ya wakulima 879 kutoka vijiji 27 wanalima vitunguu na kati ya vijiji hivyo 21 viko kandokando ya mto semi ambao ndio chanzo kikuu cha maji kwaajili ya umwagiliaji wa vitunguu.
Amesema kwa wastani vijiji vyote uzalisha wastani wa gunia 50,000/110,000 kutegemeana na hali ya mwaka husika ,na kuhusu bei amesema kwa msimu wa 20/21 ilikuwa shilingi elfu 50 hadi shilingi 110,000 kwa gunia ukilinganishwa na msimu wa 2019/20 ilikuwa shilingi elfu 20/ elfu 60 kwa gunia hatua iliyopelekea mkulima kupata kiasi cha shilingi 2,926,000 hadi shilingi 3,200,000.
Kuhusu mkakati wa namna ya kutatua changamoto hizo Rutahiwa amesema Halmashauri kwa kushirikina na wadau inafanya utaratibu wa kumwezesha mkulima kupata mikopo, kujenga kituo cha kuuzia vitunguu, kuunda vyama vya ushirika vya wakulima wa vitunguu, kuhakikisha wanunuzi wote wanatambuliwa sambamba na kuwa na vibali.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ametoa maelekezo juu ya nini cha kufanya ili kuwasaidia wakulima hao ambapo ameitaka halmashauri kufanya utaratibu wa kupata wanunuzi wa uhakika ambao wataweza kuingia mikataba na wazalishaji wa vitunguu ili kuondoa changamoto ya mikataba ya mdomoni ambayo badae inakuja kumuumiza mkulima kwani asilimia kubwa wanabadilikiwa na wanunuzi.
“Mkulima amelima, amehangaika, katoka jasho lakini yule dalali wa katikati pale kwa ujanja ujanja tu anatengeneza hela nyingi sana kuliko hata mlimaji hiki ni kitu hatutakubali tutahakikisha tunakidhibiti ili mkulima apate jasho lake …na wanunuzi ukipiga lumbesa huo mzigo unataifishwa amesema.” RC Kafulila.
Na Anita Balingilaki ,Meatu